Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

VIDEO: Hatimaye mwili wa aliyefia mikononi mwa polisi wachunguzwa

Video Archive
Mon, 1 Oct 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Moshi. Mwili wa Henry Kiwia, dereva wa daladala za Kiborlon aliyefariki dunia baada ya kuwekwa mahabusu katika Kituo Kikuu cha Polisi mjini Moshi, umekabidhiwa kwa familia kwa ajili ya mazishi baada ya kufanyiwa uchunguzi wa kitaalamu (postmorterm), katika hospitali ya Rufaa ya KCMC.

Taarifa kutoka katika familia ya marehemu zimeeleza kuwa mwili huo ulichukuliwa na polisi na ndugu kutoka Hospitali ya Mawenzi saa 4:55 asubuhi na kupelekwa KCMC ambako ulifanyiwa uchunguzi na daktari huru kutoka Arusha.

Kaka mkubwa wa marehemu, Hadson Kiwia ambaye alishiriki katika uchunguzi huo, aliiambia Mwananchi kuwa taarifa rasmi ya sababu za kifo cha marehemu itatolewa kesho.

“Kwanza tumekubaliana na polisi kwamba jina halisi la marehemu kulingana na cheti cha ubatizo ni Henry na sio Andrew na polisi wamekubali kurekebisha kwa hiyo taarifa itasomeka hivyo,” alisema.

Baada ya hatua hiyo, sasa wamejipanga kuzika Jumatatu, wakati wakisubiri taarifa rasmi za daktari.

“Tumeshiriki kwenye postmoterm na imefanywa na daktari kutoka Arusha wala sio wa KCMC au wa Mawenzi wala hafahamiani na polisi wa Moshi na tumesaini,” alieleza.

“Tumejulishwa kuwa taarifa rasmi ya kile alichokiona daktari itatoka Jumatatu (kesho) na kutakuwa na nakala tatu; moja watabaki nayo polisi, nyingine daktari na moja mahakama,” alisema.

Mwanafamilia huyo alisema wanatarajia kufanya kikao cha familia leo kuamua ama wasamehe au walipeleke suala hilo mahakamani. “Kufanyika kwa hii postmorterm hauondoi ukweli kuwa ndugu yetu alifia mikononi mwa polisi. Nini kilimuua sasa hiyo itategemea taarifa ya daktari itakayotoka Jumatatu,” alisema.

“Bahati nzuri tumepata daktari ambaye sio wa Mawenzi wala KCMC wala hafahamiani na polisi yeyote Kilimanjaro. Wametuambia watatupa tu summary (kwa kifupi) ya taarifa Jumatatu”.

Alisema hivi sasa wanaendelea na taratibu za mazishi yatakayofanyika nyumbani kwao Msaranga Moshi.

Kaka mwingine wa marehemu, Ernest Kiwia alisema walichokuwa wakipigania ni kufanyika kwa uchunguzi wa kifo kwa vile kina shaka kutokana mazingira.

Ilivyokuwa

Inadaiwa kuwa Henry alikamatwa akiwa na mwenzake Obasanjo Kitwi, jirani na Stendi ya Kiborlon Ijumaa ya Septemba 21 saa 5:00 asubuhi na polisi waliokuwa doria na kupelekwa katika Kituo Kikuu cha Wilaya.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Hamis Isah alikaririwa akisema kuwa usiku wa Septemba 23, marehemu aliwehuka akiwa mahabsu na kuanza kumwaga majihali ambayo alidai iliwalazimu polisi kuwahamishia eneo lingine mahabusu wenzake wote na kumuacha peke yake, na ndipo alipogundulika amejinyonga kwa kutumia suruali yake ya jeans.

Kauli ya RPC Issah iliwakera wanafamilia na kuamua kususia mwili huo hadi utakapofanyika uchunguzi wa kina kujua sababu za kifo cha ndugu yao, wakidai kuwa alikufa kutokana na kipigo cha polisi.

Mama wa marehemu, Haikamesia Kimambo alidai kuwa siku mwili wa mwanaye ulipotolewa mahabusu, polisi waliwafukuza hapo kituoni kitendo kinachoashiria kuwapo kwa nia ovu.

Kaka wa marehemu ,Nicholaus Kiwia alidai kushangazwa na taarifa hiyo ya RPC kuwa ndugu yao alikuwa na matatizo ya akili na kumtaka athibitishe kauli hiyo kwa kutoa uthibitisho wa daktari.

Akizungumza na gazeti Septemba 25, kaka wa marehemu, Frank Kiwia alidai kwamba alipouchunguza mwili wa mdogo wake, aliona paji la uso likiwa limepasuka na mikono ikiwa na majeraha makubwa.

“Kwenye paji la uso alikua amepasuka na mikono yake ilikua ina majeraha ya kufungwa. Shingo yake alikua imekatwa na kitu kama katani sio suruali kama polisi wanavyodai,” alidai Frank.

Tukio la mtuhumiwa huyo kudaiwa kujinyonga akiwa mahabusu, liliibua hisia tofauti kutoka kwa ndugu na baadhi ya wakazi wa mjini Moshi, wakitaka uchunguzi wa kina ufanyike ili kupata ukweli.

Chanzo: mwananchi.co.tz