Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

VIDEO: Akiwa na miaka 13 Moses ameshatengeneza ‘app’ ya elimu

Video Archive
Tue, 8 Oct 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

’Siku moja natamani kuwa mwanasayansi mkubwa hasa kwenye teknolojia ya habari na mawasiliano. Nataka nijulikane ndani na nje ya nchi yangu kutokana na utaalam wangu na hilo litafanikiwa nikifanya bidii kwenye masomo,”.

Ni maneno ya Moses Mbaga ( 13) mtoto mwenye shauku kubwa ya kuja kung’ara katika fani ya sayansi hasa upande wa Teknolojia ya habari na mawasiliano (Teham).

Tayari ameshaanza kuifanyia kazi shauku yake hiyo na kwa sasa anaingia katika orodha ya wabunifu wenye athari chanya katika jamii.

Atengeneza ‘App’

Mosea ambaye hivi karibuni alihitimu darasa la saba katika shule ya msingi Montessori iliyopo jijini Dar es Salaam, ametengeneza program ya mtandaoni (app) inayowapa nafasi wanafunzi kujisomea na kufanya majaribio.

App hiyo aliyoipa jina TestYourself au ‘Jipime’ huku akipanga kuizindua rasmi Novemba mwaka huu, ni maalum kwa ajili ya mazoezi ya masomo mbalimbali kwa wanafunzi wa shule za msingi.

Pia Soma

Advertisement
Anaeleza kuwa kwa muda mrefu amekuwa akiona changamoto ya wanafunzi kubeba mzigo mkubwa wa madaftari kwa ajili ya kujifunza shuleni au wanapokwenda kuhudhuria masomo ya ziada.

Kwa kuwa amekuwa akipendelea sana kutumia simu na tabiti, anasema siku moja akiwa mtandaoni aliona mafunzo ya namna ya kutengeneza app, akavutiwa kujifunza na huo ndio ukawa mwanzo wa kujitosa kwenye ubunifu wa masuala yanayohusu teknolojia.

“Haikuwa kitu cha muda mfupi, nilianza kujifunza taratibu na kwa msaada wa kaka yangu nikafikia kuanza kutengeneza app yangu mwenyewe mwaka 2017,”

Anasema shauku ya kuwa na ‘app’ yake mwenyewe ilimfanya kujiunga kwenye kozi mbalimbali za mitandaoni kujiongezea stadi na ujuzi hadi alipofanikiwa kufikia lengo lake.

“Ninachoamini kila kitu kinawezekana ukiwa na nia, nilijifunza kile nilichotaka na wazazi wangu walikuwa pamoja na mimi kunipa ushirikiano kufikia ndoto yangu,” anaongeza Moses mwenye ndoto ya kuja kuwa bingwa katika fani ya Tehama.

Awali anasema alikuwa na wazo la kuwawezesha wanafunzi waweze kutafuta na kupakua majaribio na mitihani ya miaka iliyopita na kujisahihisha. Hata hivyo alipokwenda Baraza la Mitihani Tanzania (Necta) kwa ajili ya kupata mwongozo, alishauriwa kuongeza baadhi ya vitu.

“Naweza kusema Necta wamekuwa msaada mkubwa kwangu. Baada ya kwenda kuwaeleza wazo langu walifurahia na wakanipa ushauri uliolenga kuboresha na hatimaye nimepata kitu kizuri ambacho kinaweza kutumiwa na wanafunzi wenzangu,”

Matumizi ya app ya ‘jipime’

Moses anasema ‘app’ yake inamwezesha mwanafunzi kufanya maswali ya mitihani ya taifa kwa miaka ya nyuma sambamba na kupata majibu yake. Anasema ni maalumu kwa wanafunzi kuanzia darasa la tano hadi la saba.

Ili kupata mitihani hiyo ikiwa katika mfumo wa nakala za kimtandao, alilazimika kupeleka maombi yake Necta ambapo alishauriwa namna ya kuboresha ubunifu wake.

Necta yavutiwa

Katibu Mtendaji wa Necta Dk Charles Msonde pamoja na kushangazwa na utundu wa Moses, anasema ubunifu wake unaweza kuwa na manufaa kwa wanafunzi wa shule za msingi nchini.

“Kwa kweli nilishangazwa na barua ya mtoto wa darasa la saba akiomba mwongozo wa kuendeleza teknolojia yake aliyoifanyia ubunifu. Nilipoiona barua hiyo nikawa na shauku ya kukutana naye na baada ya kuzungumza naye mara kadhaa nikamuunganisha kwa mkurugenzi anayehusika na masuala ya Tehama kwa ajili ya mwongozo,’’anasema.

Anaongeza: ‘’Ni jambo jema kwa wazazi kutambua vipaji vya watoto wao na kuviendeleza, watoto ndiyo kizazi cha baadaye kitakachofanikisha Tanzania kutekeleza kwa vitendo ajenda ya kuwa nchi ya viwanda.”

Kinara wa masomo

Umahiri wa Moses haushii kwenye utundu wa nje ya darasa, bali pia hata kwenye masomo ya kawaida ya darasani.Akiwa shuleni hapo aliongoza katika masomo ya Hisabati, Kiingereza, Sayansi.

Mwalimu wa somo la Tehama katika shule hiyo, Ayubu Mango anaamini Mosesa atang’ara na kuwa na mafanikio makubwa siku za baadaye.

‘’Tangu akiwa darasa la tatu niliona kitu kikubwa ndani ya huyu mtoto; alinifuata akaniambia kuwa ana tablet (tabiti) hivyo akaniomba tuwe tunawasiliana kupitia barua pepe na tukaanza kufanya hivyo hata kazi tukawa tunapeana huko,” anasema.

Baba amzungumzia

Baba yake, Rogers Mbaga anasema kuwa alikitambua kipaji cha mtoto wake tangu akiwa na umri wa miaka miwili.

“Alikuwa akipenda kuchezea simu, kuzungumza na simu tangu akiwa na miaka miwili. Alipofika darasa la tatu akaanza kufungua simu mbovu na kujaribu kutengeneza. Hapo tukaanza kumuangalia kwa jicho la tofauti,” anaeleza.

Anasema familia ilikuwa naye bega kwa bega katika kuhakikisha anafanikiwa katika kila anachojifunza na ndiyo sababu walimtafutia tabiti ili aweze kujifunza vitu vingi vinavyohusiana na teknolojia.

Chanzo: mwananchi.co.tz