Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Polisi watanda Kanisa alilosimamishwa Mchungaji Kimaro

Mch. Kimaro Asd Mchungaji Eliona Kimaro

Fri, 20 Jan 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Sakati la kusimamishwa kazi kwa Mchungaji wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri (KKKT) Usharika wa Kijitonyama, Dk. Eliona Kimaro, limeendelea kuwa gumzo huku askari wakionekana kufanya doria kanisani huko.

Juzi usiku kwenye ibada ya 'masifu ya jioni', askari polisi walionekana wakizunguka nje ya kanisa hilo wakati ibada ikiendelea ndani ya kanisa.

Hata hivyo, Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro, alipozungumza na Nipashe kuhusu suala hilo, alisema doria za askari polisi ni za kawaida kwenye maeneo mbalimbali ya jiji hilo la kibiashara.

"Nikuulize kabla ya hilo sakata, hukuwahi kuona askari wakizunguka kanisani hapo? Hizi ni doria za kawaida na haihusiani na jambo hilo," alisema Kamanda Muliro.

Ikiwa ni siku ya nne tangu kuibuka kwa mvutano huo, juzi Nipashe iliwashuhudia waumini wakiendelea kufanya ibada nje ya kanisa wakati ibada ya masifu ya jioni hufanyika ndani ya kanisa.

Wakiwa nje ya kanisa hilo, waumini hao waliimba nyimbo za kumsifu Mungu na kumwombea Mch. Kimaro.

Katika kuhakikisha usalama unaimarishwa kwenye kanisani hilo, kila aliyekuwa anaingia, getini aliulizwa majina na namba za mtaa anaotoka.

Mchungaji Kimaro alisimamishwa kuendelea na huduma ya kichungaji katika usharika huo kwa siku 60 pasi na kuwekwa wazi sababu za adhabu hiyo.

Tangu Jumanne uongozi wa Dayosisi hiyo umekuwa ukitafutwa na waandishi wa habari kuzungumzia sakata hilo bila ya mafanikio.

Katibu Katibu Muktasi aliyekutwa katika ofisi hizo jana, alimweleza mwandishi wa Nipashe kuwa viongozi wote, akiwamo Askofu wa Dayosisi hiyo, Alex Malasusa, Msaaidizi wa Askofu, Lwiza na Katibu Mkuu, Goodluck Nkini, wapo nje ya ofisi kwa ajili ya vikao.

"Viongozi wote hao hawapo, wameenda kwenye vikao nje ya ofisi, kwa hiyo huwezi kuwapata kwa sasa, ahsante na karibu tena," alisema katibu huyo.

Mkuu wa KKKT, Askofu Dk. Frederick Shoo, juzi alikaririwa na vyombo vya habari akieleza kupata habari za kusimamishwa kwa mchungaji huyo kupitia mitandao na kuwataka waumini wa usharika wa Kijitonyama na wakristo kuwa watulivu.

"Tutambue kuwa dayosisi ina vyombo vyake vya uamuzi na bila shaka jambo lenyewe linaendelea kufanyiwa kazi na dayosisi husika, baadaye sisi ambao tumepokea taarifa kama hizi tunaendelea kufuatilia na kupata taarifa zaidi kuhusu jambo hili ambalo linaonyesha limeleta usumbufu na mwitikio tofauti kutoka kwa watu wengi.

"Kubwa sana ambalo ningeomba wakristo hawa na waumini wa usharika wake, waweze kuwa watulivu wakati jambo hili linaendelea kufanyiwa kazi," alisema Askofu Shoo.

Muumini wa kanisa hilo, Judith Jude alisema jana kuwa: "Hatuwezi kutoa sadaka zetu kanisani wakati mchungaji wetu kafukuzwa kama mhalifu, tulipaswa tuambiwe ili aagwe, aende anakotakiwa kupelekwa na siyo kuondolewa wakati akiwa anaendelea na semina."

Wakati akitangaza uamuzi huo, Mch, Kimaro alisema: "Nimepewa barua ya likizo ya siku 60, kwa hiyo ninatumia fursa hii kuwaaga, kesho asubuhi atahubiri Mch. Anna na ndiye atakuwa mchungaji wenu, kwa mujibu wa barua nitarudi Machi 17 na sitakuja hapa, barua inanielekeza kuripoti makao makuu ya dayosisi."

Chanzo: www.tanzaniaweb.live
Related Articles: