Dar es Salaam. Kesi inayomkabili mwandishi wa habari za uchunguzi nchini Tanzania, Erick Kabendera imeahirishwa kutokana na hakimu mkazi mwandamizi, Augustine Rwizile kupata udhuru.
Mbali na hakimu huyo kupata udhuru, wakili wa Serikali mwandamizi, Wankyo Simon ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika na kuomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.
Simon ameeleza hayo leo Jumatatu Agosti 19, 2019 mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Agustina Mmbando
“Hakimu anayesikiliza shauri hili ambaye ni hakimu mkazi mwandamizi, Augustine Rwizile amepata udhuru,” amesema Simon.
Wakati Simon akieleza hayo, wakili wa Kabendera, Jebra Kambole ameutaka upande wa mashtaka kuhakikisha upelelezi wa shauri hilo unakamilika kwa wakati kutokana na mteja wake kutokuwa na dhamana.
"Hatuna pingamizi kuhusu kupata udhuru kwa hakimu, ila tunaomba upande wa mashtaka wajitahidi kukamilisha upelelezi kwa wakati ili kesi hii iweze kuendelea kwa sababu mteja wangu anaendelea kusota rumande kutokana na mashtaka yanayomkabili kutokuwa na dhamana,” amesema Kambole.
Pia Soma
- Lori la mafuta lalipuka nchini Uganda
- Dybala azigonganisha PSG, Juventus
- Watu 63 walipuliwa na bomu wakihudhuria harusi
Soma zaidi hapa:Wakili aibua mambo mapya kushikiliwa kwa Kabendera
>Uhamiaji Tanzania yachukua paspoti saba nyumbani kwa Kabendera
> VIDEO Mwandishi wa habari Tanzania afunguliwa kesi ya utakatishaji fedha