Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mapito ya dereva teksi aliyembeba mgonjwa wa corona yalivyofuatiliwa

Video Archive
Thu, 19 Mar 2020 Chanzo: mwananchi.co.tz

Arusha. Mapito ya dereva wa teksi ambaye alimbeba mgonjwa aliyethibitishwa kuwa na virusi vya corona, Isabela Mwampamba (46) yamefuatiliwa katika Jiji la Arusha na Wilaya ya Karatu alikopitia ili kujua watu wengine aliowabeba au aliokutana nao.

Dereva huyo, ambaye jina lake halijawekwa wazi na uongozi wa mkoa wa Arusha, alimpakia mgonjwa huyo kwenye gari lake Jumapili iliyopita kumpeleka katika Hospitali ya Mount Meru.

Juzi Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu alisema mgonjwa huyo aliwasili nchini Jumapili iliyopita kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (Kia) akitokea nchini Ubelgiji.

Akizungumza na waandishi wa habari juzi, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo alisema kuna idadi kubwa ya watu wanaopaswa kuchukuliwa vipimo kutokana na kukutana na dereva huyo kwa njia moja au nyingine baada ya kumbeba mgonjwa huyo.

Alisema dereva huyo tayari amechukuliwa vipimo na vimepelekwa Dar es Salaam kutazama kama ameathirika na ugonjwa huo .

Inaelezwa dereva huyo baada ya kumshusha abiria wake alikwenda nyumbani kwake jijini Arusha na kukaa kwa muda mrefu na watoto wake.

Habari zinazohusiana na hii

Advertisement
“Sasa baada ya kuwa muda mrefu na watoto wake ambao wengine ni wanafunzi wa Shule ya Msingi Engisengeu katika Jiji la Arusha, siku iliyofuata walikutana na watoto wengine shuleni,” alieleza Gambo.

Gambo alieleza kuwa dereva huyo baadaye alikwenda Karatu ambako alipeleka abiria katika kituo cha kulelea watoto yatima cha Mwema kilichopo Karatu.

Alisema baada ya kuwafikisha Karatu, abiria hao walizungumza na watoto wa kituo hicho na kukaa nao, kisha wakarejea Arusha.

“Tayari nimezungumza na mkuu wa wilaya ya Karatu, kufuatilia suala hilo ili awafuatilie watu wote ambao walikuwa katika kituo hicho, ili wafanyiwe uchunguzi,” alisema Gambo akifafanua kuwa maeneo yote ambayo watu waliokutana na mgonjwa huyo wamepita yatafuatiliwa.

Kituo cha watoto yatima sasa nacho kimewekwa chini ya uangalizi ili watu wote hapo wafanyiwe uchunguzi.

Gambo alisema suala hilo tayari limefikishwa katika ngazi za juu na uamuzi zaidi yanatarajiwa kuchukuliwa na serikali ili kudhibiti ugonjwa huo.

Isabela, ambaye ni mgonjwa wa kwanza kupatikana nchini Tanzania alitua nchini Jumapili kwa ndege ya Shirika la Ndege la Rwanda akitokea nchini Ubelgiji.

Alisema kwamba msafiri huyo aliondoka nchini Machi 3, 2020 na kati ya Machi 5 hadi 13 alitembelea nchi za Sweden na Denmark na kurudi tena Ubelgiji na kabla ya kurejea nchini Machi 15.

Ummy alieleza kuwa mgonjwa huyo ambaye ni Mtanzania alikaguliwa uwanja wa ndege Kia lakini hakugundulika kuwa na joto kali kuashiria ugonjwa huo ila alianza kujisikia vibaya alipofika hotelini.

“Kwa mujibu wa maelezo yake alianza kujisikia vibaya alipofika hotelini ndipo alipoamua kujitenga na watu, kisha kwenda hospitali ya rufaa ya mkoa ya Mount Meru,” alisema.

Ummy alieleza Sampuli za vipimo vyake zilipelekwa Dar es Salaam katika maabara ya taifana kuthibitika kuwa ana virusi vya corona.

Chanzo: mwananchi.co.tz