Kocha Mkuu wa Geita Gold, Fred Minziro amejiweka kando na timu hiyo baada ya kile kilichoelezwa kushindwana baina yake na uongozi wa timu hiyo.
Minziro amesema amekaa kando kutokana na timu hiyo kumkatalia matakwa yake ya kumlipa kiasi cha fedha alichowatajia katika mechi mbili zilizosalia za Ligi Kuu Bara msimu huu.
“Mkataba wangu umeisha tangu Mei 28, niko nje ya mkataba nikijihudumia kwa kila kitu hivyo nikawaambia wanipe pesa kidogo kwa ajili ya kumaliza hizo mechi mbili na siwezi kuwatajia pesa kubwa sababu mimi niko na timu mwaka wa tatu sasa, lakini wakanijibu hawana kiasi hicho.
“Basi mimi nimeondoka zangu, niko Dar es Salaam naendelea na mambo mengine maana kwa tafsiri fupi unaweza kusema hawakutaka labda niendelee kwenye mechi hizi mbili na uzuri nimezungumza nao, tumemalizana vizuri,” amesema Minziro.
Alipotafutwa Ofisa Habari wa Geita, Samwel Dida amesema: “Hizi mechi mbili ziko nje ya mkataba wake, tukamwomba amalizie hizi dakika 180, akatupa utaratibu wake wa malipo, tuliona hatuwezi kumudu na yeye akawa na msimamo wake basi tukamalizana.”
Dida alisema kwa sasa kikosi chao kipo chini ya kocha wa timu ya vijana, Choke Abeid ambaye amesimamia mechi ya juzi waliyofungwa mabao 3-1 na Ihefu na ndiye atakayemalizia mechi yao ya mwisho dhidi ya Mtibwa Sugar.
Alifafanua pia, kulingana na hali iliyopo sasa baada ya kushindwana na Minziro, imekuwa ngumu kufahamu kama watakua na kocha huyo msimu ujao au la.