Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kauli ya CCM kuhusu Magufuli kumlipia faini mchungaji Msigwa

Video Archive
Fri, 13 Mar 2020 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Hamphrey Polepole amesema uamuzi wa  mwenyekiti wa chama hicho, Rais John Magufuli kumlipia faini ya Sh38 milioni mbunge wa Iringa Mjini (Chadema), Mchungaji Peter Msigwa ili atoke gerezani haupaswi kuchukuliwa kisiasa.

Amesema aliyemlipia faini mchungaji Msigwa ni Rais  Magufuli kwa sababu binti wa kiongozi mkuu huyo wa nchi ameolewa katika familia  ya mbunge huyo.

Jana Alhamisi Machi 12, 2020 Rais Magufuli kupitia wasaidizi wake walieleza kulipa  kiasi hicho cha fedha, ndugu wa Mchungaji Msigwa kuchangishana Sh2 milioni na kukamilika Sh40 milioni alizotakiwa kulipa mbunge huyo.

Hata hivyo, Chadema walisema walikuwa wameshalipa faini ya Mchungaji Msigwa na kubainisha kuwa hawakuwa wakifahamu chochote kwamba amelipiwa, kama angekuwa amelipiwa mahakama ingewarejeshea fedha zao.

Mchungaji Msigwa ni kati ya viongozi nane wa Chadema ambao pamoja na aliyekuwa Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk Vicent Mashinji Jumanne Machi 10, 2020 walihukumiwa kulipa faini ya Sh350 milioni au kwenda jela miezi mitano baada ya kutiwa hatiani kwa makosa 12 kati ya 13 yaliyokuwa yanawakabili.

Washtakiwa hao wakiongozwa na mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe walilazimika kwenda jela baada ya kushindwa kukamilisha taratibu za kulipa faini hiyo waliyohukumiwa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Habari zinazohusiana na hii

Advertisement
Baada ya hukumu hiyo iliyosomwa na Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba, Chadema walianza kuchangisha kutoka kwa wanachama wao na watu wa kada mbalimbali ili kupata kiwango hicho.

Hadi leo asubuhi Ijumaa Machi 13, 2020 viongozi wa Chadema waliotoka jela ni katibu mkuu wa chama hicho, John Mnyika; naibu katibu mkuu-Zanzibar, Salum Mwalimu; mbunge wa Tarime Mjini, Ester Matiko.

Wengine ni mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche; mchungaji Msigwa, mbunge wa Kawe, Halima Mdee na Ester Bulaya (Bunda). Mbowe bado yupo jela.

Dk Mashinji alitoka Jumatano baada ya kulipwa faini ya Sh30 milioni na CCM. Mchakato wa kumlipia faini Dk Mashinji uliongozwa na Polepole.

“Kwa lugha nyingine Rais Magufuli ni mkwe wa mchungaji Msigwa. Familia ya Msigwa imekaa,  ilikuwa ikihangaika kuchangisha fedha za kumnusuru na kifungo na habari hizi zimezungumzwa kifamilia zikimhusisha Rais Magufuli,” amesema Polepole.

Amesema Rais Magufuli alitoa mchango huo na kuwatuma wasaidizi wake, akiwamo katibu huyo wa uenezi sambamba na kuweka utaratibu mahakamani, benki hadi gereza la Segerea ili kumtoa mbunge huyo.

“Ni bahati mbaya jambo hili limechukuliwa kisiasa, ndugu Magufuli ni binadamu kama wengine ni baba na mwana familia. Kama Msigwa hakutaka kutambua aliyemsaidia ni nani au wapotoshaji wanataka kulibadilisha jambo na kuleta habari nyingine lakini mchakato wa kumtoa umekamilika.”

“Ushahidi upo bayana kabisa muda ambao tumelipa benki fedha anazodaiwa Msigwa na kupata kibali kutoka mahakamani. Rais Magufuli anaamini maendeleo hayana chama,” amesema Polepole.

Katika maelezo yake, Polepole amesema katika mchakato huo Rais Magufuli  hakutizama itikadi  licha ya kufahamu mchungaji Msigwa yupo Chadema, “alitizama changamoto za  kimaisha na kifamilia.”

Kwa mujibu wa Polepole, Rais Magufuli ametimiza wajibu wake kama mwanafamilia, huku akitaka ujumbe huo uwafikie watu wote wenye dhamira njema na mapenzi kwa Taifa na wasigeuze itikadi za kisiasa kuwa uwanja wa mapambano.

Chanzo: mwananchi.co.tz