Nchi

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Kijamii

Lifestyle

SIL

MenuNchiPeopleSiasa
George Simbachawene

Watu Maarufu Tanzania

Siasa

George Simbachawene

Waziri wa Mambo ya Ndani

Chawene Pfd
Tarehe ya Kuzaliwa:
1968-07-05
Mahali pa Kuzaliwa:
Tanzania

George Boniface Simbachawene amezaliwa tarehe 5 mwezi Julai mwaka 1968, katika wilaya ya Mpwapwa, iliyopo mkoani Dodoma.

Ni mwanasiasa kutoka chama cha Mapinduzi CCM, amekuwa mbunge wa Bunge la Tanzania tangu mwaka 2005 hadi sasa 2021, amehudumu kwa miaka 16 sasa kama muwakilishi wa wananchi wa jimbo la Kibakwe.

Kwa sasa, kiongozi huyu ni Waziri wa Mambo ya Ndani, nikusogeze karibu na historia ya Waziri huyu, upate kumjua kiundani.

ELIMU

Alianza elimu ya msingi mwaka 1978 katika Shule ya Pwaga iliyoko wilayani Mpwapwa. Alisoma shule hiyo hadi mwaka 1982 na mwaka uliofuata alihamia Shule ya Msingi ya Mahomanyika iliyoko mkoani Dodoma ambako alihitimu darasa la saba mwaka 1982.

Elimu ya Sekondari aliipata kuanzia mwaka 1985 hadi 1988 katika Shule ya Sekondari ya Ufundi Mazengo, pia ya mkoani Dodoma. Mwaka 1989 hadi 1993 alikwenda jijini Arusha na kusoma Chuo cha Ufundi cha Arusha ambako alitunukiwa Cheti cha Ufundi (TFC).

Mwaka 2001 hadi 2005 aljiunga na Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT) ambako alitunukiwa shahada ya kwanza ya sheria (LLB).

SIASA NA KAZI

Mwaka 2007 alishiriki mafunzo ya kazi na taratibu za uendeshaji wa Kamati za Kibunge kwenye Bunge la Westminister na kutunukiwa cheti na mwaka 2010 alitunukiwa cheti kingine baada ya kuhitimu mafunzo juu ya bunge hilo.

Uzoefu wa kazi wa Simbachawene unaweza kuwekwa kwenye makundi manne, kwanza ni uzoefu wa kazi za kitaalamu, pili wa kazi za kibunge, tatu ni uzoefu wa kazi za uwaziri na mwisho ni uzoefu wa utendaji ndani ya CCM.

Baada ya kuhitimu na kubobea katika masuala ya ufundi, ilimchukua miaka miwili kabla ya kuajiriwa na kampuni ya mabasi ya Urafiki, tawi la Dodoma mwaka 1995. Alikuwa kondakta, meneja wa kitengo cha ufundi na ofisa usafiri. Mwaka 1997 hadi 1998 aliajiriwa na Kituo cha Mafunzo ya Ufundi cha Future World akiwa mwalimu. Kati ya kipindi hicho hadi mwaka 2000, alifanya kazi kama mkurugenzi mtendaji wa shirika la kiislamu la Muzdalifa linalojishughulisha na masuala ya misaada.

Mwaka 2005 Simbachawene, akiwa na miaka 37, aliachana na ‘ukonda’ akaamua rasmi kuitafuta ofisi kubwa ambayo watu wengi waliokuwa naye hawakudhani kama angeliweza kuifikia. Alijitosa kwenye kinyang’anyiro cha ubunge kwa tiketi ya CCM, akamwangusha aliyekuwa mbunge wa Kibakwe na hivyo kupeperusha bendera ya chama hicho katika uchaguzi wa mwaka huo.

Mshindani wake mkubwa alikuwa Benson Kigaila wa Chadema na Gabrile Elias Masinjisa wa NCCR Mageuzi. Matokeo ya mwisho yalimpa Simbachawene ushindi wa asilimia 86.1 (kura 37,359), Benson akifuatia kwa asilimia 12.8 (kura 5,542)

Baada ya ubunge wa miaka mitano, Simbachawene alitupa tena karata yake mwaka 2010, na akaibuka kidedea kwenye kura za maoni za kata 13 kati 16 baada ya kupata kura 8,824 huku mpinzani wake, Aggrey Galawika akiwa na kura 2,537 na hivyo, Simbachawene akapata ridhaa ya kuiwakilisha CCM.

Kwa mara ya pili alikumbana na Kigaila wa Chadema, lakini akamshinda tena kwa kupata kura 22,418 sawa na asilimia 77.12 dhidi ya kura 5,585 sawa na asilimia 19.21% za Kigaila.

Mwaka 2015, Simbachawene alitupa ndoano yake jimboni Kibakwe kwa mara ya tatu akashinda kwenye kura za maoni kwa kupata kura 18,159 akiwaacha mbali washindani wake sita ambao ni Gabriel Mwanyingi (kura 6,900), Akrei Mnyang’ali (kura 3,563) na Amani Bendera (kura 410).

Kwenye Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 25 mwaka 2015, alipambana na Mzinga William wa Chadema na kumshinda kwa kura 37,327 sawa na asilimia 81,55 dhidi ya kura 8,447 za mpinzani huyo.

Baada ya kushinda Ubunge mwaka 2010, Simbachawene aliteuliwa na Rais Kikwete kuwa Naibu Waziri wa Nishati na Madini kuanzia Mei 2012 hadi Januari 2014 alipohamishiwa Wizara ya Nyumba na Makazi akiendelea na unaibu.

Januari 2015 alipandishwa na kuwa Waziri wa Nishati na Madini akichukua nafasi ya Profesa Sospeter Muhongo aliyejiuzulu kutokana na sakata la uchotwaji fedha kwenye Akaunti ya Tegeta Escrow.

Hayati Magufuli alipotangaza baraza lake mwaka 2015, Simbachawene alipangwa Tamisemi akiwa waziri.

Ndani ya CCM alianza kama mwanachama na kiongozi wa matawi, likiwamo la Chuo cha Ufundi Arusha kati ya mwaka 1990 hadi alipomaliza. Pia alikuwa mjumbe wa kamati ya siasa ya wilaya kati ya mwaka 2002 – 2005.

Januari 23, 2020 chini ya uongozi wa Hayati Magufuli, aliteuliwa kuwa Waziri wa Mambo ya ndani akichukua nafasi ya Kangi Lugola.

Uchaguzi wa mwaka 2020, alipita kwa kishindo mara dufu, hadi sasa naendeleza gurudumu la kuwaongoza wananchi wa Kibakwe.

Katika kutangaza Baraza jipya la Mawaziri, Hayati Magufuli alimuacha Waziri huyu katika nafasi yake ndani ya Wizara ya ya Mamboya ndani, hii inaonesha kuwa utendaji wake wa kazi ni wa kuvutia na wa haki.

sifa nyingine kubwa ya Simbachawene ni subira. Watendaji ambao wamefanya kazi naye Wizara ya Nishati na Madini , TAMISEMI na Wizara ya Mambo ya ndani wanamsifu kuwa ni mtu mwenye kuuliza kila jambo analotaka kuamua, lakini pia anawasikiliza sana watendaji na wataalamu.

Haiba hii huenda ndiyo imesababisha hadi leo hii Simbachawene ameendelea kuwa na ‘namba ya uhakika’ kwenye mabaraza ya mawaziri hata katika serikali zinazokuja kwa gia ya “kasi” Wakati alipoachiwa Wizara ya Nishati na Madini kutokana na waziri wake kujiuzulu, wengi walidhani angeanza kwa gia ya kufanya maamuzi lukuki ambayo ndani yake lazima kungekuwa na makosa mengi, badala yake aliongoza kwa utulivu na subira kubwa hadi kumaliza kipindi chake.

Akiwa katika Wizara ya Mambo ya Ndani, anapambana vikali na matukio ya uhalifu pamoja na ugaidi kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi nchini.

TanzaniaWeb