Nchi

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Kijamii

Lifestyle

SIL

MenuNchiPeopleSiasa
Bernald Membe

Watu Maarufu Tanzania

Siasa

Bernald Membe

Historia ya Bernald Membe

Pope 2
Tarehe ya Kuzaliwa:
1953-11-09
Mahali pa Kuzaliwa:
Lindi

Benard Membe alizaliwa Novemba 9, 1953 katika Kijiji cha Rondo-Chiponda, Wilaya ya Lindi hivyo atatimiza miaka 62, Novemba mwaka huu. Ni mtoto wa pili kati ya saba wa familia ya Mzee Kamillius Anton Ntanchile na mama Cecilia John Membe. Hivi sasa ni Mbunge wa Jimbo la Mtama mkoani Lindi na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.

Membe alianza elimu ya msingi mwaka 1962 katika Shule ya Rondo - Chiponda na alihitimu mwaka 1968, baadaye alikwenda kuendelea na masomo ya sekondari katika Seminari ya Namupa na kusoma kidato cha kwanza na nne kati ya mwaka 1969-1972. Alisoma kidato cha tano na sita katika Seminari ya Itaga mkoani Tabora kuanzia mwaka 1973 hadi 1974.

Maandiko kadhaa yanaonyesha kuwa Membe aliwahi kusomea upadri kwa miezi kadhaa kabla hajajiunga na Seminari ya Itaga akiwa mmoja kati ya vijana 11 walioshawishiwa na alichaguliwa kujiunga na Seminari Kuu ya Peramiho, Songea.

Ndoto ya Membe kusomea upadri huko Peramiho ilianza kuyumba polepole baada ya matokeo ya kidato cha nne kutoka yakionyesha kuwa amefaulu vizuri. Hali hiyo ilimfanya Askofu Mkuu wa Jimbo la Mtwara wakati huo, Maurus Libaba (marehemu), amshawishi ahamie Itaga Seminari kusoma kidato cha tano na sita.

Membe alijiunga na JKT, kwa mujibu wa sheria. Baadaye alifanya kazi serikalini miaka miwili ili kutekeleza Azimio la Musoma ambalo lilitaka watu wote waliomaliza kidato cha sita kufanya kazi miaka miwili kabla ya kujiunga na masomo ya chuo kikuu.

Baada ya kumaliza JKT, Membe hakukumbuka tena upadri, badala yake aliajiriwa kwenye Ofisi ya Rais na kufanya kazi kwa miaka sita ndipo alijiunga Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kusomea Shahada ya Sayansi ya Siasa na Utawala wa Umma kuanzia mwaka 1980 hadi alipohitimu mwaka 1984.

Japokuwa ufaulu wake ulikuwa wa daraja la kwanza, alikataa “ofa” ya kuendelea na jahazi la Chuo Kikuu cha Dar es Salaam la kuwa mhadhiri msaidizi kwa sababu Ikulu ilimtaka arejee kazini mara baada ya masomo.

Moja ya majukumu aliyoisaidia Ikulu ni pamoja na kuchambua masuala ya Usalama wa Taifa na aliifanya kazi hiyo kwa mafanikio.

Membe alijiendeleza kitaaluma kwa kujiunga na Chuo Kikuu cha Johns Hopkins, Marekani mwaka 1990 akisomea Shahada ya Uzamili (MA) ya Uhusiano wa Kimataifa na kuhitimu mwaka 1992.

Baada ya kuhitimu pamoja na kuisaidia Ikulu kipindi kirefu, Membe alihamishiwa Wizara ya Mambo ya Nje mahali alipokaa kwa miaka tisa (1992–2000) akishughulika na kazi ngumu ya kuwashauri mabalozi, kabla ya kuamua kujiunga katika siasa za moja kwa moja.

Membe ni mume wa Dorcas Masanche tangu mwaka 1986 na wamefanikiwa kuwa na watoto watatu, mmoja ni wa kike na wawili ni wa kiume.

Mbio za ubunge

Safari yake kisiasa ilianza mwaka 2000 kwenye Uchaguzi Mkuu alipoomba ridhaa ya ubunge Jimbo la Mtama mkoani Lindi kwa tiketi ya CCM. Uchaguzi ulipofanyika, CCM ikaibuka na ushindi ikiviacha vyama vingine kwa mbali. Membe akachaguliwa na wananchi wa Mtama wakati huo akiwa na miaka 47.

Mwaka 2005, CCM ilimrejesha kutafuta ushindi wa Mtama kwa mara ya pili na bahati yake ikawa nzuri kwa sababu Isack Wolfgans Ndaka wa TLP na Said Hamis Mtepa wa CUF hawakumpa upinzani mkubwa hivyo alitetea ubunge wake kwa kupata asilimia 79.3 ya kura.

Rais Jakaya Kikwete alimteua kuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani kuanzia Januari 2006 hadi Oktoba 2006 alipomhamishia Wizara ya Nishati na Madini Oktoba 2006 ambako alishikilia wadhifa wa unaibu waziri kwa mwaka mmoja hadi Novemba 2007.

Desemba 2007, Membe alipanda ngazi na kuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa akichukua nafasi ya Dk Asha-Rose Migiro na alidumu katika wizara hiyo hadi awamu ya kwanza ya JK ya miaka mitano ilipokamilika.

Membe aliendelea kuomba ridhaa mwaka 2010, ambao ulikuwa mwepesi zaidi. Aliongeza ushindi kutoka asilimia 79.3 za mwaka 2005 hadi asilimia 81.76 mwaka 2010 kwenye Jimbo la Mtama.

Baada ya kuwa mbunge kwa kipindi cha tatu, Rais Kikwete alimteua tena kuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, nafasi ambayo ameendelea kuwa nayo hadi sasa.

Mbio za urais

Miaka 15 ya Membe kuwatumikia wana Mtama imekoma baada ya yeye mwenyewe kutangaza rasmi kuwa hatakuwamo kwenye msafara wa wasaka ubunge jimboni humo Oktoba mwaka huu. Kuaga huko kumetafsiriwa kwamba anakwenda kuisaka ofisi ya juu zaidi, Magogoni.

Wakati anawaaga wana Mtama tayari kumekuwa na ushahidi kuwa amekuwa akijipanga kwa ajili ya azma hiyo muda mrefu uliopita na si vibaya kusema yeye ni kati ya wasaka urais kupitia CCM ambao wamefanya maandalizi ya muda mrefu.

Membe ni mmoja wa makada zaidi ya 40 wa CCM waliojitokeza kuwania kupitishwa na chama hicho kwenye nafasi ya urais wa JMT.

Membe alikuwa mpinzani mkuu wa Edward Lowassa kada aliyekuwa anapewa nafasi kubwa ya kuwa mrithi wa Rais Jakaya Mrisho Kikwete, na ambaye baada ya kutopitishwa CCM alihamia Chadema, japo baadaye alirudi tena CCM.

Membe alikuwa miongoni mwa “tano bora” pamoja na Magufuli, January Makamba, Amina Ali na Asha Rose Migiro.

Hata hivyo hakufanikiwa Kupita kwenye mchuano huo. aliyefanikiwa kupita ni Hayati John Pombe Maghufuli.

Membe ni mwanadiplomasia aliyebobea na ana nguvu inayodhihirika kimataifa. Amekuwa katika Wizara ya Mambo ya Nje akiwa mtumishi wa kawaida, kwa miaka minane na baadaye waziri wa wizara hiyo hiyo kwa takriban miaka mingine minane.

Uzoefu huo wa miaka 16 kwa ujumla umemrusha hadi kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Mawaziri wa Nchi za Jumuiya ya Madola (CMAG) Novemba 2013 huko Sri Lanka. Kabla ya hapo, wadhifa huu, mara nyingi, ulikuwa ukishikiliwa na viongozi kutoka nje ya bara la Afrika.

Nguvu ya pili ya Membe iko katika uzoefu wake kwenye masuala ya utendaji ndani ya serikali na usalama wa nchi. Kwa kifupi Membe ni kachero mzoefu na ameifanya kazi hiyo tangu alipomaliza kidato cha sita na ilifika wakati akawa hadi msaidizi wa mkuu wa Idara ya Usalama wa Taifa. Kwa hiyo, anaijua nchi hii vizuri na ana taarifa za kutosha za mambo mengi nyeti yaliyojiri tangu enzi hizo.

Kingine kinachompa nguvu ni uungwaji mkono ndani ya CCM. Huyu jamaa anaungwa mkono na kundi kubwa ndani ya CCM na naweza kusema anavutana na makada wawili hivi, kati ya wasaka urais. Amekuwa akigombea na kushinda nafasi ya ujumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM tangu mwaka 2007 na tena akachaguliwa mara ya pili mwaka 2012 kwenye Mkutano Mkuu wa Nane wa CCM (akishinda kupitia kundi la kifo) kwa kupata kura 1,451 nyuma ya Stephen Wasira, Mwigulu Nchemba na January Makamba tena kukiwa na shinikizo kubwa kutoka kwa mahasimu wake kisiasa.

Membe ana nguvu isiyoweza kubezwa katika misimamo kwenye masuala ya msingi. Mfano, amekuwa akitetea waziwazi suala la uraia pacha bila kujali kuwa chama chake kimekuwa hakilitaki suala hilo tangu enzi za Mwalimu Nyerere.

Pia Membe amekuwa akisimama kidete kumtetea Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe wakati mataifa ya Magharibi yakiwa yamemtenga na kutomtambua bila kusahau kupinga sera za Magharibi dhidi ya Palestina (misimamo mingine ni ya nchi na amekuwa akiisimamia ipasavyo).

Membe ana nguvu nyingine kimataifa kwa maana ya kukubalika na kupanga mipango inayoweza kuleta tija na kulinufaisha Taifa.

Ni katika uongozi wake wa Wizara ya Mambo ya Nje, ndipo Serikali ya Tanzania ilipofanikiwa kuwakaribisha viongozi wa dola zinazoongoza dunia; Rais Xi Jinping wa China na Barack Obama wa Marekani tena kwa mapokezi ya kiwango cha juu.

Udhaifu wake

Moja ya udhaifu wa Membe ni upole uliozidi. Ni mpole sana; mpole kupita kiasi. Watu wa karibu yake wanasema kwamba kuna wakati anakuwa na huruma hata katika masuala yanayohitaji avae ngozi ya simba.

Kwa hali ya nchi yetu ilipofikia, Taifa linahitaji rais mkali kidogo na ikiwa ataendeleza upole wake huo utakuwa udhaifu mkubwa mno kumkabidhi dola.

Udhaifu mwingine wa Membe ni kushindwa kuelewana na maadui wake kisiasa. Wakati Rais Kikwete anaisaka Ikulu, ni Membe na washirika wengine waliosimama kidete na kufanya kazi pamoja hadi akashinda.

Miaka michache baadaye aliokuwa nao kundi moja wakageuka kuwa maadui wa kutupwa na kila mmoja ameshindwa kurudi chini na kuondoa “uhasama” uliopo. Huu ni udhaifu kwa kiongozi na mwanadiplomasia wa kimataifa.

Taswira nyingine ya udhaifu wa Membe ni utata. Membe ni kati ya viongozi watata.

Mei 2014, akiwa bungeni Dodoma aliutangazia umma na hata kunukuliwa na vyombo vya habari vya kimataifa akiishutumu Rwanda kwamba inawafadhili waasi wa kikundi cha M23 kinachosumbua Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na alidai kuwa M23 ni raia wa Rwanda.

Matamshi hayo yalikuwa hatari na tata kuwahi kutamkwa na mwanadipolomasia wa ngazi ya kimataifa kama Membe.

Katika suala la rada, pia Membe alituonyesha utata mkubwa. Mei 2011, alikataa uamuzi wa Kampuni ya BAE kuilipa Tanzania Dola za Marekani 29.5 milioni kupitia mfumo wa “msaada” (sadaka) akisema msaada hauwezi kuruhusiwa kama malipo hayo yatafanyika, akasisitiza kuwa “…watu hawa wamechanganyikiwa na wanajaribu kujitoa kwenye kashfa hii na kusukuma mzigo kwa serikali ili dunia iamini kwamba Tanzania ni nchi ya kifisadi na haiaminiki”.

Pamoja na kauli hiyo ya kuwashughulikia BAE, Membe hakuwahi kuwalaumu wala kuwashutumu wale wote waliohusika na rushwa katika kashfa hiyo.

Hata Mei 2012, Mkurugenzi wa Takukuru, Dk Edward Hoseah alipotamka kwamba hakuna Mtanzania aliyehusika kwenye kashfa ya ununuzi wa rada na hata habari hizo ziliporipotiwa na Gazeti la ‘Daily News’ la Machi 31 mwaka huo, bado Membe hakujitokeza hadharani akiwa Waziri wa Mambo ya Nje kupinga kauli hiyo au kutoa maoni yake juu ya wizi huo. Unaweza kujiuliza, nini ulikuwa uwajibikaji wa Membe katika jambo kubwa kama hili?

Nini kinaweza kumfanya apitishwe

Jambo moja kubwa linamlofanya Membe atazamwe kama mmoja wa watu wanaoweza kuvuka kigingi cha CCM na hatimaye kuteuliwa kuwa mteule wa urais ndani ya CCM ni ukaribu wake na Rais Kikwete.

Mpaka sasa hakuna anayeweza kuthibitisha kama Kikwete anampigia chapuo Membe, lakini kama taarifa hizo ni kweli, basi zitamrahisishia njia.

Kingine kinachoweza kumvusha Membe ni kutoandamwa na kashfa. Hata alipokuwa Naibu Waziri wa Nishati na Madini huku kashfa ya Richmond ikinguruma, Membe hakuhusishwa hata kidogo na hadi sasa ameendelea kuwa mmoja wa viongozi ambao hawatajwi katika kashfa mbaya za rushwa. Taswira hii iliyojijenga kwamba yeye anaweza kuwa miongoni mwa viongozi wasiopenda ufisadi na wanaokataa kujihusisha nao, inaweza kumfanya aonekane kuwa chaguo la CCM.

Kitu kingine kinachoweza kumbeba ni kusimamia ukweli. Membe ana rekodi ya kusimamia ukweli hata kama utamuumiza na kuna nyakati anafanya hivyo bila kujali hatari zinazoweza kumkabili.

Mathalani, mwaka 2001/2002 aliposimama kishujaa dhidi ya aliyekuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Utawala Bora, Dk Hassy Kitine kuhusu kashfa ya kutumia fedha za serikali kumtibu mke wake, Saada Mkwawa nje ya nchi kwa kiwango cha Dola za Marekani 63,000.

Pamoja na Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), chini ya Kaimu Mwenyekiti Richard Ndasa kuandika barua Wizara ya Afya ili kumsafisha Kitine na mkewe, Membe alisimama kwa miguu yote na kuonyesha ubadhirifu huo kwa uwazi hadi Bunge likachukua hatua za kinidhamu dhidi ya Kitine na genge lake.

Nini kinaweza kumwangusha?

Kama kuna jambo lililo wazi linaloweza kumwangusha Membe katika safari yake ya kuitafuta Ikulu ni makundi.

Kiongozi huyu amekwishajijengea kundi kubwa ndani ya CCM kwa kipindi kirefu ambalo linapambana na makundi hasimu.

Ikiwa CCM itahitaji kuwa na mgombea ambaye hana makundi na atakiunganisha chama, Membe anaweza kuwekwa pembeni.

Kitu kingine kinachoweza kumtupa Membe ni misimamo yake katika baadhi ya mambo ambayo kuna nyakati yamekwenda hata kinyume na mtazamo wa chama chake.

Kuna wakati Membe huthubutu kufanya mambo ambayo wenzake hawayapendi hasa katika nyanja za kimataifa. Ikiwa CCM itahitaji Rais anayesikiliza zaidi sauti za chama chake, Membe anaweza kuwa nje.

Asipopitishwa (Mpango B)

Membe asipopitishwa na chama chake nadhani atawekeza nguvu kwenye shughuli za kidiplomasia kwa maana ya diplomasia ya kimataifa na kusaidia jumuiya ya kimataifa katika utatuzi wa migogoro mbalimbali kutokana na uzoefu alio nao.

Lakini pia anaweza kutumia ujuzi na uzoefu wake kufanya shughuli za ujenzi wa chama chake katika ngazi za juu kwa sababu watu wa aina yake ni “tunu” muhimu.

Na mwisho anaweza kutumika katika kushauri masuala ya ulinzi wa nchi yetu ukizingatia kwamba amekuwa kwenye Idara ya Usalama wa Taifa kwa kipindi kirefu.

Membe ni mmoja wa wanasiasa wenye ndoto za juu mno hapa Tanzania. Ndoto zake hizo zinasababisha kambi nyingine zinazosaka urais ndani ya CCM zisilale usingizi.

Ana ufuasi mkubwa miongoni mwa wana CCM na ni mtu mashuhuri kwamba akikabidhiwa nafasi ya uteule ndani ya CCM, hakuna atakayeshtuka. Nadhani alianza harakati za urais kipindi kirefu na amekwishajipanga vya kutosha.

Yeye ni miongoni mwa wana CCM wachache wenye uwezekano wa kupenya lile “chekecheo kuu”. Namtakia kila la heri katika safari yake hiyo.

Hayo yote yalikuja kubailika baaada ya Membe kupata Mtafaruko ndani ya CCM na kupelekea kuitwa kwenye kamati ya Maadili. Kukingana na makosa aliyokutwab nayo chama kiliamua kumvua uwanachama.

Julai 2020 alikwenda kujiunga na Chama cha ACT Wazalendo chini ya mwenyekiti wao Zitto Kabwe. ilipofika mwaka 2020 Membe aligombe urais kupitia ACT wazalendo. lakini Chama cha CCM kilibuka mshindi.

Kufikia Januari mosi mwaka 2021, Membe alitangaza hadharani kwa amejiudhuru rasmi uwanachama wa ACT Wazalendo akiwa kijijini kwake Rondo Chiponda mkoani Lindi.

Mwananchi