Katika maisha omba sana bahati. Kuna vitu huwezi kuvipata hadi uwe na bahati tu. Wakati mshambuliaji John Bocco akitangazwa Kustaafu soka, Clatous Chota Chama bado anagombewa na Simba na Yanga huku, Saido Ntibanzokinza hakuna anayemtaka.
Inafurahisha kuona Bocco anastaafu wakati Chama akigombewa. Inasikitisha kuona mfungaji bora wa Simba kwa msimu wa pili mfululizo, Ntibazonkiza anaachwa na hakuna klabu inayomtaka.
Omba sana bahati. Unaweza kuwa na vigezo vyote lakini kama hauna bahati kuna mahali utakwama. Ntibazonkiza ni mchezaji mwenye wasifu bora kwenye soka pengine kuliko mchezaji mwingine yoyote. Amecheza Ufaransa, Yanga, Simba msimu mmoja na nusu na amefunga mabao mengi.
Pamoja na kufanya hivyo kwa msimu wa pili mfululizo, hakuna anayejali wala anayestuka. Kila mtu anaona ni sawa tu Simba kumuondoa. Ndiyo maisha yalivyo.
Ligi Kuu Bara bado umri sio kigezo kikubwa cha mchezaji kutokufanya vizuri, wachezaji wenye umri mkubwa wanatamba. Wachezaji wetu ni kama wanachelewa kukomaa. Wengi wanaanza kuwa imara baada ya miaka 25. Wachezaji wengi wanaofanya vizuri ni wale wenye umri mkubwa.
Bado mchezaji kama Ntibazonkiza angeweza tu kubaki Simba na angetoa mchago. Lakini ana bahati? Hilo ndiyo swali. John Bocco anastaafu, Chama bado anagombewa na klabu za Kariakoo, Ntibazokinza hakuna anayemtaka. Bahati. Bahati. Bahati.
John ni mmoja. Ndiye mshambuliaji bora mzawa kucheza ligi yetu kwa misimu 15 ya hivi karibu. Hakuna kama yeye. Labda hatukumpa Heshima anayostahili. Labda tulimchukulia poa lakini ukweli utabaki pale pale, hakuna kama Bocco kwenye nchi yetu.
Zama hizi zilikuwa na Bocco. Ukiingia kwenye mtandao, utaona Bocco amezaliwa Mwaka 1989. Ni kijana tu wa miaka 34. Hata kama Umri wa wachezaji wengi wa Kiafrika unachekechwa lakini sioni tatizo. Angetaka kucheza, bado Bocco anaweza kucheza na kufunga.
Mahitaji ya Simba, Yanga na Azam ni makubwa lakini Bocco hashimdwi kucheza Tabora United au Pamba Jiji FC. Taarifa zinaeleza anakwenda kuwa Kocha wa timu za Vijana pale Simba. Sio mbaya. Ni maamuzi mazuri lakini Mwamba wa Lusaka bado anagombewa pale Kariakoo. Bado Simba na Yanga wanapigana vikumbo kuitaka Saini yake. Ndiyo Maisha yalivyo.
Chama anatajwa kuzaliwa mwaka 1991. Kimahesabu ni tofauti ya miaka miwili tu Kati yake na Bocco. Pamoja na yote hayo, umri ni namba tu. Hakuna matumizi makubwa ya nguvu kiasi cha wenye miaka 30 kushindwa kucheza. Bocco angetaka bado angeweza kucheza. Pale hakuna mshambuliaji mzawa anayefikia uwezo wa Bocco. Pale Yanga naona Clement Mzize anakuja lakini bado anasafiri ndefu ya kufika kwa Bocco.
Moja kati ya shida kubwa za Simba baada ya kuachana na Meddie Kagere, Bocco na Chris Mugalu ilikuwa ni kupata mshambuliaji mwingine wa uhakika. Alikuja Moses Phiri na Jean Baleke. Kuna namna walianza kutatua tatizo lakini ghafla Phiri Kiwango kikashuka.
Ghafla Baleke akaondoka Simba. Saido akaja na kubalisha upepo. Ligi yetu mshambuliaji mzuri ni yule mwenye uwezo wa walau kufikisha mabao 10 ya ligi kwa msimu. Ni wachache sana kwenye ligi yetu wana uwezo huo. Saido ni miongoni mwao. Ni kweli uwezo wake umepungua laini wengi hawamuwezi.
Bado anauwezo mkubwa wa kuamua mechi kuliko wachezaji wengi Vijana. Huyu ni aina ya wachezaji ambao angeweza kubaki na Simba wakapata pakuanzia. Changamoto ya kuwaondoa wachezaji wa aina yake ni kuwa na uhakika na mchezaji mpya anayekuja kuwa kufunga na kuisaidia timu kuliko Sido.
Simba wanalaumiwa sana miaka ya hivi karibuni baada ya usajili wao kusuasua, lakini hili ni jambo la kawaida sana. Usajili una mambo mengi. Ni kama Kamari.
Manchester United, Chelsea, Liverpool pamoja na kuwa na mifumo ya Kisasa kabisa ya usajili, kuna namna na wao pia wanachemsha. Unahitaji kuwa na wachezaji walau wanaokupa uhakika wa mabao 10 kwenye ligi yetu. Simba naona wakicheza kamari kubwa zaidi msimu ujao.
Kwa idadi ya wachezaji wanaoachana nao kuna dalili za kuona sura nyingi sana mpya. Bado haikupi uhakika wa moja kwa moja sura mpya zitaleta matokeo mapya.
Mmoja wa wachezaji ambao kila dirisha la usajili lazima atikise ni Chama. Kila dirisha la usajili huwa anahusishwa na kwenda Yanga lakini msimu ukianza anacheza Simba. Labda mara hii kunaweza kuwa na utofauti.
Uvumi wa kwenda Yanga umekuwa mkubwa kuliko wakati mwingine wowote. Hakuna ubishi, Chama ana akili kubwa sana ya mpira. Akili yake inafanya kazı kubwa sana uwanjani na ni aina ya wachezaji wanaoweza kwenda timu yotote na akawa chaguo la kwanza.
Uzuri wa Chama ni anapokuwa kwenye kikosi chenye wachezaji wanaoweza kukaba. Hataki shida. Kazi kubwa ni kwenye kufanya maamuzi eneo la mwisho la Ushambuliaji. Chama hana mfanano.
Anatajwa sana kwenda Yanga. Kuna balaa linakuja. Wachezaji wanaocheza kwenye staili kama ya Chama, huwa hawachoki mapema. Anaweza kucheza kwa muda mrefu sana. Hawa wanatumia zaidi maarifa kuliko nguvu. Yanga wakimpata watakuwa wamelamba Dume.
Wakati mwingine ni vyema kukubali kuanza upya. Chama amefanikiwa sana kwenye kulinda thamani yake. Kazi yake uwanjani imekuwa na mwendelezo. Amekuwa na mchango mkubwa sana kwenye mashindano ya Kimataifa. Ni moja ya usajili bora kwa wachezaji wa Kigeni hapa nchini.
Bocco anastaafu, Ntiba hatakiwi lakini Chama bado thamani yake ni ya juu. Sio watu wote wamebahatika kuwa na thamani hiyo kwa wakati wote. Kila msimu mpya, Chama ameendelea kutajwa kugombewa na wababe wote wa soka letu. Kıla nikifikiria Bocco amestaafu, hakuna anayemtaka Ntibazonkiza na Chama bado anagombewa, naishia kusema maisha yanahitaji pia bahati.