Kufuatia kufanikiwa kutinga robo fainali kwa kishindo cha mabao 7-0 dhidi ya Horoya, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Simba, Salim Abdallah ‘Try Again’ amewachimba mkwara watani zao wa jadi Yanga kwa kusema linapokuja suala la mechi za mashindano ya Afrika Simba ndio wakali wa shughuli hizo, wengine wanaiga.
Simba ambao ni wawakilishi pekee wa Tanzania katika mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika juzi Jumamosi ilifanikiwa kutinga hatua ya robo baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 7-0 dhidi ya Horoya AC ya Guinea.
Ushindi huo uliifanya Simba kuwa timu ya pili kutoka kundi C la mashindano hayo kukata tiketi ya kucheza robo fainali baada ya kufikisha pointi 9 na kuendelea kusalia kwenye nafasi ya pili ya msimamo nyuma ya Raja Casablanca.
Akizungumza nasi, Try Again alisema: “Kwa niaba ya uongozi, wachezaji, benchi la ufundi na mashabiki wote tunamshukuru Rais Dk. Samia Suluhu kwa motisha anayotoa katika michuano ya Ligi ya Afrika kwa timu za hapa nyumbani.
“Ushindi wetu dhidi ya Horoya umeonyesha wazi kuwa linapokuja suala la mashindano ya kimataifa Simba ndio wenye shughuli hizi, wengine wanaiga lakini sisi ndio waanzilishi.”