Simba imeanza mipango ya msimu ujao ikitaka kuboresha kila eneo ili kuhakikisha inarejea kwenye makali yake na kwa kuanzia itafanya maboresho kwenye benchi lake la ufundi kwa kuondoa baadhi ya watu na kushusha wataalamu wapya.
Uongozi wa Simba kwa nyakati tofauti umekaa vikao na kila mtaalamu aliye katika benchi la ufundi la timu hiyo na kutathimini hatima yake ndani ya kikosi kwa kuzingatia maelewano dhidi ya wenzake, sehemu alipofaulu na alipofeli na kupata mwanga wa wapi pa kuanzia.
Kocha msaidizi wa timu hiyo, Juma Mgunda huenda msimu ujao asiwe kwenye benchi la ufundi la Wekundu hao kutokana na kile kilichoelezwa ni maelewano hafifu na bosi wake, Mbrazil Roberto Oliveira ‘Robertinho’.
Hivyo Simba inataka kumuondoa Mgunda ili kumuachia mikoba kamili Robertinho.