Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Simba yatua kwa beki wa Yanga

Boka Simba yatua kwa beki wa Yanga

Wed, 26 Jun 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Dili la Simba limebuma baada ya kutaka kumnyampia beki wa FC Lupopo, Chadrack Boka, ambaye hawakujua kama tayari ameshamalizana na Yanga.

Boka ni mchezaji wa kwanza kusaini Yanga baada ya uongozi wake kukubali kumuuza mchezaji huyo ambaye alibakiza mkataba wa mwaka mmoja na kikosi hicho.

Iliripotiwa kuwa, Mkongomani huyo atakwenda kuwa mrithi wa beki wa kushoto Joyce Lomalisa ambaye amemaliza mkataba wake ndani ya Yanga.

Boka mwenye uwezo wa kucheza kama winga, pia amekuwa na kiwango bora katika klabu hiyo kwani ilitaarifiwa kuwa mashabiki vinara wa Lupopo waliposikia anaondoka walifanya maandamano kuzuia kuondoka kwake.

Akizungumza nasi kwa njia ya simu kutoka DR Congo, Boka amesema: "Sikuwahi kufanya mazungumzo nao (Simba) kabla lakini kocha wangu mmoja alinitafuta akaniambia watu wa Simba wanakutafuta. Akawapa namba zangu wakanipigia lakini sikuwa na maongezi nao marefu.

"Niliwaambia kwamba tayari nimeshasaini mkataba wa awali Yanga, wakaniambia nisiende huko watajua namna ya kumaliza hilo, nikawambia wawatafute wenyewe Yanga au wamtafute rais wa Yanga yeye ndiye aliyekuja huku kuongea na mimi."

Katibu Mkuu wa FC Lupopo, Donat Mulongoy ameeleza kuwa; "Kweli tulipokea simu za watu wa Simba wanasema wanajua kwamba Boka bado ni mchezaji wa Lupopo na wanataka kutupa pesa mara mbili ya ile Yanga wanataka kutoa kama tukikubali kufanya nao biashara.

"Tumewaambia hakuna namna mambo yanaweza kubadilika kwa kuwa kila kitu kimemalizika muda mrefu kama wao bado wanamtaka mchezaji wasubiri afike Tanzania wataongea na watu wa Yanga."

Kiongozi huyo ameongeza kwamba: "Lupopo hatuzuii kufanya biashara zipo timu ambazo hatuwezi kufanya nazo biashara hata za mchezaji mmoja na hizo zipo hapa Congo, lakini nje ya hapa tunaweza kufanya biashara na timu yoyote.

"Kwa hili la Boka hakuna njia tunaweza kupindua mambo kwa kuwa kila kitu kinamalizika vizuri, Yanga walikuja hapa tukaongea na rais wao na baadaye wetu Bwana Kyabula (Jacques) amekuja Tanzania, wakatuma tena mtu hapa tukamaliza hiyo biashara kitu kinabakia hapa ni Yanga kumleta mchezaji huko watakapoona inafaa."

Licha ya hayo Yanga bado haijamtangaza mchezaji huyo wala haijaanza kuagana na wachezaji wake ambao hawatakuwa nao msimu ujao huku mipango ya kufanya hivyo ikipangwa kuwa ni Julai Mosi, mwaka huu.

Simba inapambana kusaka beki wa kushoto ambaye atasaidiana na Mohamed Hussein 'Tshabalala' ambapo awali ilielezwa kuwa na mpango wa kumchukua Joyce Lomalisa aliyemaliza mkataba Yanga, lakini dili lake likazuiwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi, Mohammed Dewji 'Mo'.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live
Related Articles: