Uongozi wa Simba umeshitukia mbinu za wapinzani wao Wydad Casablanca ya nchini Morocco kuwatoa mchezoni huku wakielekeza akili na nguvu zao katika mchezo huo watakapokutana.
Timu hizo zinatarajiwa kuvaana leo Jumamosi kwenye Uwanja wa Mkapa Jijini Dar es Salaam katika mchezo wa kwanza wa hatua ya Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Wydad Casablanca mara baada ya kutua walilalamikia kupewa uwanja mbovu wa kufanyia mazoezi wa Gymkhana uliopo Posta, Dar.
Wydad ambao wamefikia Serena Hotel jijini Dar, juzi usiku walifanya mazoezi mepesi wakiwa nchini baada ya kuwasili mchana wakitokea Morocco.
Baada ya mazoezi mepesi walidai kuwa uwanja walioutumia ni mbaya kutokana na eneo la kuchezea kutokuwa zuri huku Kocha Mkuu wa timu hiyo, Juan Carlos akiingia hofu ya wachezaji wake kupata majeraha.
Akizungumza nasi, Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally alizungumzia hilo kwa kusema kuwa: “Hizo wanazozitumia Wydad Casablanca ni mbinu za kimchezo zenye lengo la kututoa mchezoni.
“Kama uongozi tupo imara kabisa tukiendelea na maandalizi ya mchezo huo, kwani uwanja huo wanaoutumia ndio ambao unatumia na timu zote za nje zinazokuja, kikubwa wafahamu tunataka ushindi hapa nyumbani kabla ya kurudiana kwao.”