Klabu ya Simba imetangaza kuwaongezea mikataba wachezaji wake wazawa, Kibu Denis Prosper, Israel Patrick Mwenda na Mzamiru Yassin Selemba kuendelea kusalia klabuni hapo hadi mwaka 2026
Akizungumzia hilo, Meneja Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally amesema kuwa haikuwa kazi rahisi kuwabakisha wachezaji hao ambao wamekuwa mhimili mkubwa wa kikosi hicho msimu uliopita.
“Katika wachezaji ambao hautakaa usikie wana matatizo ya utovu wa nidhamu, ni Mzamiru Yassin. Kama tungelemaa kidogo Kibu denis tungemkosa safari hii. Kibu awe anaumwa, awe awe usingizini ama kitu chochote yupo tayari kwenda kuipigania Simba.
“Na safari hii Kibu atafanya makubwa makubwa sana kwa sababu mahitaji yake yote ya kimkataba tumeyatimiza na amekwenda mapumziko Marekani.
“Isarel Mwenda naye haikuwa rahisi, vijana wamejanjaruka wanafahamu haki zao, mazungumzo sio mepesi, akifika anasoma mkataba na Israel shule imo.
“Hawa wachezaji watatu walikuwa kwenye first eleven msimu uliopita, kwa hiyo wakiondoka maana yake msimu unaanza ukiwa na pungufu ya wachezaji watatu. Kuna mchezaji anakuja, straika mrefu kuliko goli, haruki, mpira ukipigwa tu imo na ana nguvu vibaya mno,” amesema Ahmed.