Uingozi wa Simba umeweka wazi kuwa mara baada ya kupoteza mchezo wao wa kwanza wakiwa nyumbani katika Uwanja wa Mkapa dhidi ya Raja Casablanca, safari hii hawataki utani watakapokutana na Vipers wakiwa nyumbani katika uwanja huo huku wakisema kuwa timu hiyo wataipelekea pumzi ya moto.
Simba katika mchezo wa kwanza wakiwa nyumbani dhidi ya Raja Casablanca ya Morocco walipoteza kwa kufungwa mabao 3-0, mchezo wao wapili wakiwa nyumbani wanatarajiwa kucheza leo Jumanne dhidi ya Vipers.
Akizungumza nasi, Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally alisema: “Mchezo wa kwanza ni kweli tulipoteza tukiwa nyumbani dhidi ya Raja Casbalanca tukafungwa mabao 3-0.
“Safari hii niwaambie tu Vipers wamejichanganya kwani tutawapelekea pumzi ya moto na hakika lazima tupate matokeo mazuri ya kuwafurahisha Wanasimba wote ambao wamekata tamaa.
“Bado tuna michezo miwili ya nyumbani, lazima tuitumie vizuri nafasi hii kwani naamini Simba kufika robo fainali ni kawaida kwake, hivyo Wanasimba tunawaomba mje kwa wingi kushangilia chama lenu ili tuwapige vizuri Vipers kwa Mkapa,” alisema kiongozi huyo.