Wakati wakiwa wanasubiri droo ya robo fainali kujua watavaana na timu gani kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika, kiungo mshambuliaji wa Simba, Saidi Ntibazonkiza ‘Saido’ amechimba mkwara mzito kuwa wako tayari kwa mpinzani yeyote ambaye watakutana naye kwenye hatua hiyo.
Simba usiku wa kuamkia Jumamosi walikuwa na kibarua kizito cha kuwavaa Raja Casablanca ya Morocco katika mchezo wa kukamilisha ratiba yak und C la mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika huku Simba akiambulia kipigo cha bao 3-1, lakini timu hizo mbili tayari zilikuwa zimefuzu hatua ya Robo fainali.
Mara baada ya kukamilika kwa hatua ya makundi, Aprili 5, mwaka huu Shirikisho la Soka Afrika (CAF), linatarajiwa kufanya droo ya robo fainali ya mashindano hayo ambapo Simba watavaana na mmojawapo wa vinara wa kundi A, B au D.
Akizungumza nasi, Saido alisema: “Malengo makubwa ya timu kwa msimu huu ni kuvuka hatua ya robo fainali ambayo timu imefanikiwa kucheza kwa mafanikio katika misimu ya karibuni, hivyo tunataka kwenda hatua zaidi kwenye hatua ya nusu fainali au zaidi.
“Tunafahamu tutakutana na timu ngumu zaidi katika hatua hii kwa kuwa tutacheza na timu iliyoongoza kundi, lakini tunaamini kuwa tuna nafasi ya kufanya makubwa zaidi na kucheza nusu fainali.”