Simba juzi usiku iliizamisha Ruvu Shooting kwa kuishusha daraja rasmi baada ya kuifumua mabao 3-0 kwenye mechi ya Ligi Kuu Bara iliyopigwa Uwanja wa Azam Complex Chamazi, huku kocha mkuu wa timu hiyo, Roberto Oliveira Robertinho akikiri wamemaliza hovyo msimu na wanaenda kujipanga upya.
Robertinho ambaye mara tu baada ya kutambulishwa na Simba kutoka Vipers ya Uganda alijinasibu kwamba anataka kurejesha taji la ubingwa wa ligi kutoka kwa Yanga, lakini sasa amebadili gia akisema mambo yameenda sivyo na sasa anaenda kusuka kikosi kwa ajili ya msimu ujao akitamba mnyama atatisha.
Mbrazili huyo alitua Simba katikati ya msimu akichukua mikoba iliyoachwa na Zoran Maki aliyeanza msimu na timu hiyo kabla ya kuikacha na kutimkia Misri na juzi baada ya mechi na Ruvu aliliambia Mwanaspoti, amewashukuru viongozi, wachezaji na mashabiki wa Simba kwa kujitoa kwa ajili ya timu yao licha ya kwamba haukuwa msimu bora kwao lakini wanaenda kujipanga upya.
“Kila mmoja ndani ya Simba ametimiza wajibu wake kwa kiasi kikubwa, kilichotokea ni matokeo tu ya kimchezo na sasa tumekubali tumeanguka msimu huu, lakini sio kwa misimu mingine. Tunajua tumekosea wapi, tunafanya tathimini ya kila eneo na mwisho wa siku tutakuja na mapinduzi makubwa,” alisema Robertinho na kuongeza;
“Wachezaji wetu hawapaswi kulaumiwa, kila mmoja alifanya anachoweza kwa uwezo wake na sasa tuache maneno tuungane kujenga Simba imara itakayofikia malengo kwa msimu ujao.”
Aidha Robertinho alizungumzia usajili wa wachezaji wapya na watakaondoka kwa kusema bado ni mapema, lakini amepanga kufanya mabadiliko makubwa.
“Ni mapema kulizungumzia hilo lakini kiukweli tutafanya mabadiliko makubwa. Nafanya kazi kwa misingi ya taaluma yangu, na kama unavyojua soka ni mchezo wa wazi hivyo nitaendelea kuwa na kundi la wachezaji ambao wanajituma na kufanya kazi kwa moyo mmoja lakini hata tutakaowasajili natumaini wataishi kwenye msingi huo,” alisema.
Simba imebakiza mechi mbili za ligi tu dhidi ya Polisi Tanzania na Coastal Union lakini hata hivyo, kimahesabu ni kama imemaliza msimu kwani itamaliza katika nafasi ya pili kwa matokeo yeyote yale.
Mataji iliyoyakosa Simba msimu huu ni lile la Ligi ya Mabingwa Afrika ikiishia robo fainali, Ligi Kuu, Kombe la Shirikisho la Azam(ASFC), Mapinduzi na Ngao ya Jamii na sasa inajipanga na CAF Super Cup, ambayo ni mipya na imepangwa kuchezwa kwa mara ya kwanza mwishoni mwa mwaka huu.
Licha ya Robertinho kuwa mgumu kuanika panga lake la Msimbazi, lakini Mwanaspoti linafahamu ameshaanza kusajili wachezaji wapya akiwamo beki wa pembeni Yahya Mbegu kutoka Ihefu na inazungumza na kiungo Sospeter Bajana wa Azam, mbali na nyota wengine kutoka Vipers.
Pia Mwanaspoti limedokezwa kwamba Simba itaachana na baadhi ya nyota wake wa sasa akiwamo Joash Onyango, Moses Phiri, Augustine Okrah, Mohamed Ouattara, Ismael Sawadogo, Peter Banda, Mohamed Mussa, Habib Kyombo, Jonas Mkude, Gadiel Michael na Beno Kakolanya.