Mshambuliaji wa Simba, Mzambia, Moses Phiri, amesema wapinzani wao Horoya AC, ndiyo wana tiketi yao ya kufuzu hatua robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu.
Kauli hiyo ameitoa mara baada ya Simba kufanikiwa kupanda hadi nafasi ya pili katika msimamo wa Kundi C, wakiwa na pointi 6, huku Raja Casablanca wakifikisha 12 na kuwa timu ya kwanza kufuzu.
Ushindi wa bao 1-0 walioupata Simba juzi dhidi ya Vipers kwenye Uwanja wa Uganda, ndiyo umefufua zaidi matumaini hayo, huku wakihitaji kuifunga Horoya, Machi 18, mwaka huu ili kufikia malengo hayo.
Akizungumza nasi, Phiri alisema katika mchezo dhidi ya Horoya watacheza kufa au kupona kuhakikisha wanashinda ili wafuzu hatua ya robo fainali.
“Kwanza tulihitaji pointi tatu dhidi ya Vipers, baada ya hapo tunaangalia mchezo unaofuata tutakaocheza hapa nyumbani dhidi ya Horoya.
“Sio mchezo mwepesi kwetu, lazima tujiandae na tuweke malengo ili tufanikishe malengo yetu ya kufuzu, ni mchezo ambao utaamua hatima yetu ya kufuzu robo.
“Kama wachezaji tutahakikisha tunacheza kufa au kupona kufanikisha malengo yetu ya kufuzu robo fainali, Horoya tumewaona katika mchezo uliopita, hivyo tutaingia uwanjani kimbinu zaidi na kikubwa kupata ushindi,” alisema Phiri.