Kocha wa Simba, Roberto Oliveira 'Robertinho' humwambii kitu kuhusu kiraka wa timu hiyo, Erasto Nyoni kwani licha ya kumkubali majukumu yake uwanjani, bado anataka kumpa cheo kingine ambacho kitafanya aendelee kusalia kikosini.
Nyoni mwenye umri wa miaka 35, alisajiliwa na Simba msimu wa 2017-2018 akitokea Azam akiwa sambamba na Aishi Manula, John Bocco na Shomary Kapombe na kwa misimu minne kati ya mitano aliisaidia timu hiyo kubeba taji manne la Ligi Kuu Bara, mataji mawili ASFC na kuifanya Simba itishe.
Awali kulikuwa na taarifa huenda mchezaji huyo mkongwe akawa mmoja ya watakaotemwa kutokana na umri, lakini imeelezwa kocha Robertinho amezungumza na mabosi wa klabu hiyo, akiwataka wambakize Nyoni kwa namna yoyote ile.
Inadaiwa kocha huyo ametoa sababu ya kumbakisha kiraka huyo anayemudu kucheza kama beki na kiungo kuwa ni ukomavu wa akili aliyonayo kwa mchezaji huyo, akiamini anaweza akawa kiongozi mzuri wa dhidi ya wenzake.
"Kocha anataka Nyoni awe kiongozi wa wachezaji wenzake, anamuona akili yake imekomaa na ana maamuzi anayoweza akawasaidia wengine kukaa kwenye njia sahihi, kutokana na umri wake, amesisitiza wasije wakamuachia aondoke," kilisema chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya Simba kilichoongeza;.
"Nyoni ni mchezaji anaweza akawakemea wadogo zake wanapofanya sivyo,hana mambo mengi ya kumfanya awe na nidhamu mbovu, jambo ambalo kocha anaona kuwepo kwake kikosini kutaongeza utulivu kwa wengine kuzingatia nidhamu na kujituma kwenye majukumu yao."
Nyoni ambaye mkataba wake unaishia msimu huu, kutokana na kauli ya kocha viongozi inawalazimu kukaa chini kufanya mazungumzo ya kumuongezea mkataba mpya.
"Ukiachana na nidhamu ya Nyoni ambayo ipo wazi, kocha anapenda uwezo wake anaoweza akacheza zaidi ya nafasi moja, anaona amejitunza kwa umri wake angekuwa hana nidhamu angekuwa ameishaondoka kwenye mstari.
"Suala la Nyoni tunalishughulikia na tumeona kocha ana hoja, kikosi hakiwezi kujaa vijana pekee."