Imeelezwa kuwa Simba ipo katika taratibu za mwisho za kukamilisha usajili wa kiungo mkabaji wa Rivers United ya nchini Nigeria, Joseph Onoja mwenye umri wa miaka 24.
Simba ipo katika mipango ya kuinasa saini kwa ajili ya msimu ujao ili kuiboresha safu ya kiungo ambayo inachezwa na Sadio Kanoute, Mzamiru Yassin, Jonas Mkude na Ismail Sawadogo.
Timu hiyo, imepanga kukifanyia maboresho makubwa kikosi chao katika msimu ujao ili kifanye kweli katika Ligi Kuu Bara na mashindano ya kimataifa.
Mmoja wa Mabosi wa Simba, amesema kuwa kiungo huyo atakuja kuchukua nafasi ya Sawadogo ambaye ameshindwa kuonyesha kiwango bora.
Bosi huyo alisema kuwa uongozi umefikia hatua ya kumsajili kiungo huyo baada ya kumfuatilia kwa ukaribu akicheza katika michuano ya kimataifa tangu msimu uliopita na huu.
Aliongeza kuwa kama mazungumzo yatakwenda vizuri kati ya menejimenti ya kiungo na uongozi wa Simba, basi huenda akavalia jezi zenye rangi nyeupe na nyekundu msimu ujao.
“Sawadogo usajili wake umeonekana kufeli baada ya kushindwa kuonesha ubora wake katika baadhi ya michezo ambayo alipewa nafasi ya kucheza.
“Hivyo uongozi upo katika mipango ya kumsajili kiungo mwingine mwenye uwezo zaidi ya kwake na anayepewa nafasi kubwa ni Onoja.
“Mazungumzo tayari yameanza ya kimyakimya kuhakikisha wanaipata saini yake, kwani wanataka kuiboresha safu ya kiungo ukabaji,” alisema bosi huyo.
Meneja Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally alizungumzia hilo la usajili na kusema kuwa: “Benchi letu la ufundi kwa kushirikiana na uongozi hivi sasa unafuatilia kwa karibu michuano hii ya kimataifa Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirisho Afrika.
“Lengo ni kuwaona wachezaji wenye vigezo na uwezo mkubwa watakaokuja kuingozea nguvu Simba katika msimu ujao, tumepanga kufanya usajili mkubwa.”