Meneja wa mshambuliaji kinara wa Simba, Jean Othor Baleke raia wa Congo DR, Clovis Mashisha amekiri kuwa mchezaji huyo ana mkataba na Klabu ya TP Mazembe hivyo yuko Simba kwa Mkopo.
Mashisha amesema hayo wakati akifanyiwa mahojiano maalum na chombo kimoja cha Habari nchini Tanzania baada ya tetesi kusambaa kuwa Baleke si mchezaji wa Simba badala yake yupo klabuni hapo kwa mkopo na muda wowote Mazembe wanaweza kumchukua mchezaji wao.
“Baleke akiwa na miaka 20 amefanya makubwa TP mazembe na Timu ya Taifa ya Congo, kwa hiyo sio mchezaji wa kawaida. Kule kwetu mashabiki wa Mazembe wanamuita Baleke ‘Samatta’.
“Hii ni kwa sababu wanakumbuka kazi nzuri aliyoifanya Mbwana Samatta pale TP Mazembe kabla ya kutimkia KRC Genk ya Ubelgiji, kwa hiyo alipokwenda pale wakasema basi tumepata Samatta mpya,” amesema Mashisha.
Ikumbukwe kuwa, msimu wa mwaka 2015/16, Samatta aliisaidia Mazembe kushinda Kombe la Mabingwa Barani Afrika huku yeye akiibuka kama kinara wa kupachika mabao katika Ligi hiyo kubwa Afrika.
Haikuishia hapo tu, Samatta pia alifanikiwa kunyakua Tuzo ya Mchezaji Bora wa Afrika wa Mwaka kwa wachezaji wanaocheza ndani ya Bara la Afrika akiwabwaga mastaa kibao.
Kwa upande wa Baleke ambaye alisajiliwa na Simba kwa mkopo katika dirisha dogo la usajili msimu huu, tayari ameshacheza mechi 14 na kufunga mabao 14 kwenye michezo mbalimbali ya kimashindano.
Hii imewafanya viongozi na mashabiki wa timu hiyo kumuamini na kuamini kuwa wametibu tatizo la safu ya ushambuliaji lilikokuwa likiwasumbua tangu kuondoka kwa Meddie Kagere na Chris Mugalu.