Kocha Mkuu wa Simba SC, Roberto Oliveira ‘Robertinho’ ameweka wazi kuisuka timu hiyo katika usajili wa dirisha kubwa ili iwe bora kwenye msimu ujao kwenye mashindano wanayoshiriki.
Simba SC kwa msimu wa pili mfululizo imemaliza bila kuwa na taji lolote, jambo ambalo linamlazimu kocha huyo kuhakikisha anakuwa na kikosi kipana ambacho kitahimili kucheza mashindano tofauti kwa mafanikio.
Robertinho amesema msimu ujao anataka kuwa na wachezaji bora na wazuri kwa kila eneo ili kuwe na usawa kwenye kikosi chake wakati anapokosekana anayeanza kikosi cha kwanza, lakini kupeana muda wa kupumzika na timu kuwa salama.
“Nahitaji wachezaji wawili kwenye kila nafasi ndani ya kikosi changu, hii itafanya timu yangu iwe na usawa mzuri hata mmoja anapokosekana, mwingine anakuwa bora,” amesema Robertinho.
Amesema kwa sasa anavutiwa na namna ambavyo timu yake ilivyo na uwiano mzuri wa wachezaji vijana na wazoefu ambao anaona kabisa inazidi kuwapa fursa vijana kuwa bora.
“Mfano hapa nina Banda (Peter), hata nikimpa nafasi ya kuanza nakuwa na amani kwa sababu ni mchezaji mzuri ndani ya uwanja, anaweza kuanzisha mashambulizi.
“Kibu (Denis) na yeye ni mzuri kwa hiyo kupitia wachezaji hawa vijana watatu naiona kesho nzuri ya Simba SC kwenye kikosi changu kiukweli. Tunatakiwa kuwa bora uwanjani.”
“Sakho (Pape) pia nina furaha naye hata mchezo uliopita alikuwa bora na kufunga mabao mawili, akiwa na mpira anakuwa mwepesi kupeleka mashambulizi na ndicho ambacho kinahitajika kwenye mpira wa kisasa,” amesema.
Robertinho amefunguka zaidi na kusema Sakho anapokuwa anacheza kwa spidi na kuingia ndani ya boksi inakuwa rahisi sana kwake kufunga na ndio kitu ambacho anataka iwe.