Zamani ilikuwa ngumu kumuona mchezaji kutoka Bongo anakwenda mapumziko nchi kama Marekani, Ufaransa, Dubai na nyingine ila kwa sasa linawezekana kwani Ligi ya Tanzania imeanza kulipa vizuri na wachezaji wanapata mikwanja ya kwenda huko kula bata katika kipindi cha mapumziko kama ilivyo kwa mastaa tofauti ulimwenguni.
Unavyosoma hapa, staa wa Simba, Kibu Denis yupo zake Marekani. Anakula bata na washikaji zake wa karibu pamoja na familia yake kwa ujumla baada ya kuvuta mkwanja wa maana kutoka Simba.
Ndio. Pesa za Simba ndizo zinampa jeuri ya kujivinjari katika mitaa ya Miami pale Marekani lakini ni matokeo ya jasho alilovuja kwa misimu mitatu ndani ya Wekundu wa Msimbazi hao.
Kwa sasa Kibu ni miongoni mwa mastaa wazawa ndani ya Simba wanaolipwa mshahara mzuri lakini pia ni mchezaji ambaye hashikiki. Yaani ukitaka kumnunua lazima uvunje banki kweli kweli.
Hiyo ni baada ya mkandaji huyo kusaini mkataba mpya Simba wenye thamani isiyopungua Sh300 milioni. Ndiyo Kibu ameweka kibindoni mzigo huo kama pesa ya usajili.
Lakini pia kwenye mkataba wake mpya atakuwa anakunja mshahara na marupurupu mengine ambayo ukijumlisha haipungui Sh10 milioni kwa mwezi. Sio kitu kidoga.
Muda unakwenda mbio, Kibu Denis anatakiwa kuziacha bata za Miami na kurejea Bongo kabla ya Julai 5 mwaka huu ili ajiunge na Simba kwenda Ismailia, Misri kwaajili ya kambi ya msimu mpya maarufu 'preseason'.
Hapo ndipo Mkandaji ataanza rasmi kuutumikia mkataba wake mpya na ndipo sehemu ambayo kuna mtego unaomsubiri staa huyo wa timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars.
Ukirudi nyuma kidogo utakumbuka Kibu aligeuka Lulu sokoni miezi miwili iliyopita. Yanga iliweka mzigo mezani, Ihefu ikapania kuvunja benki ili kumpata staa huyo lakini mwisho wa yote akaamua kusalia Simba.
Wapo waliohoji zaidi kutakiwa na Yanga, wengine wakajiuliza Kibu huyuhuyu ndiye wa kulipwa na kusaini mkataba kwa pesa nyingi hivi? Wote hawakupata majibu na sasa wanatarajia kuyapata msimu ukianza.
Mkataba huo mpya ni mtihani mgumu kwa Kibu. Ni saini aliyoweka mwenyewe lakini akizingua inaweza kugeuka kuwa shubiri kwake licha ya kwamba hakuna anayeombea iwe hivyo.
Ni wazi mashabiki wengi wa Simba hawamkubali kivile Kibu lakini kwa sasa ni kama wamefunika kombe mwanaharamu apite. Wanamsikilizia msimu uanze wapate cha kusema. Wajikumbushe mamilioni anayolipwa Kibu kisha walinganishe na anachokifanya uwanjani. Ni Mtihani mgumu kwa Mkandaji.
Kibu hapaswi kuwapa mashabiki muda wa kukumbuka pesa Simba iliyotoa kumsainisha mkataba mpya, wala mshahara anaolipwa.
Anapaswa kupiga kazi kwelikweli. Anatakiwa kujiongeza na kuwa na matokeo chanya uwanjani ili mashabiki wasahau pesa zao, wamuimbe kama mfalme Msimbazi.
Kibu siyo mchezaji wa kupewa muda tena. Misimu mitatu ya kwanza pale Simba imetosha. Sasa ana mtihani ambao anatakiwa kufanya vizuri zaidi na akifaulu basi ataimbwa ipaswavyo.
Mashabiki hawatakuwa tayari kuvumilia msimu mzima Kibu akifunga mabao mawili pekee kama alivyofanya msimu uliopita ambao alifunga bao moja tu kwenye Ligi Kuu Bara na akatupia jingine moja kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika. Hizi sio takwimu za mchezaji anayecheza eneo la kushambulia.
Hawatamvumilia akifunga mabao mawili tu kama alivyofanya msimu wa 2022-23. Takwimu zake bora tangu atue Simba zilikuwa katika msimu wake wa kwanza ambapo alifunga mabao manane na kutoa asisti nne.
Ni zamu ya Kibu kugeuka mwokozi wa Simba. Kwa sasa hatasifiwa tena kwa kivuli cha 'Upambanaji na Uparanganaji', atasifiwa kwa kuibeba Simba kwenye nyakati ngumu na zile bora. Anatakiwa kuwa bora muda wote kama atakuwa fiti na hicho ndicho Wanasimba wanahitaji.
Ni mchezaji ambaye anauwezo wa kufanya hivyo kwani anauhakika mkubwa wa kupata muda mwingi wa kucheza ndani ya kikosi cha Simba. Tangu ametua Msimbazi mwaka 2021 hakuna kocha amembania kucheza, amepewa nafasi na kila mwalimu aliyepita pale Msimbazi.
Matarajio ni hali hiyo kuendelea kwani makocha waliopita Simba kwa nyakati tofauti waliliambia Mwanaspoti kila kocha anapenda mchezaji aina ya Kibu kwa maana ya nidhamu, kujituma na kufuata maelekezo kwani ndiyo nguzo ya mafanikio.
Mkandaji anatakiwa afungue ukurasa mpya ndani ya Simba wenye sura mpya yenye mitazamo chanya juu yake. Akishindwa, amekwisha kwani mashabiki wa soka nchini tabia zao zinajulikana.
Hawakuweza kumvumilia John Bocco licha ya kuwa mfungaji bora wa muda wote kwenye ligi akiwa amecheka na nyavu mara 154. Waliona amechoka na kuamua kumstaafisha kwa nongwa na ujanja ujanja wa mjini. Hivyo hivyo kwa Kipa Juma Kaseja, alistaafishwa licha ya kuwa alikuwa bado mbichi.
Hivyo ndivyo soka la Bongo linavyoenda. Yaani Kivyetu, Kivyetu. Kibu anapaswa kuishi maisha mapya ndani ya Simba kwa akili vinginevyo huenda mkataba mpya ukawa mchungu kwa staa huyo wa zamani wa Mbeya City, Geta Gold na Kumuyange FC ya Ngara.