Kiwango kikubwa anachoendelea kukionyesha, kiungo mshambuliaji wa Simba, Kibu Denis katika Ligi ya Mabingwa Afrika kimempa ugumu Msenegal, Pape Ousmane Sakho.
Kibu amekuwa akiipa mchango mkubwa Simba katika michuano ya kimataifa akiwa ameingia moja kwa moja katika kikosi cha kwanza cha Kocha Mkuu wa timu hiyo, Mbrazil Roberto Oliviera ‘Robertinho’.
Kiungo alianza kuingia katika kikosi cha kwanza dhidi ya Horoya AC mchezo uliopigwa nchini Guinea kabla ya kurudiana juzi kwenye Uwanja wa Mkapa Jijini Dar es Salaam.
Taarifa ambazo tumezipata, Sakho ana kibarua kigumu cha kuingia katika kikosi cha kwanza cha Simba kutokana na nafasi ambayo amekuwa akipewa Kibu kila mara na kocha Robertinho.
Aliongeza kuwa Kibu tayari amefanya kikao na Robertinho akimtaka kutobweteka na badala yake kuongeza bidii na kutimiza majukumu anayompa ya kufunga na kuwatengenezea nafasi za kufunga wachezaji wenzake.
“Licha ya mashabiki kumbeza, Kibu lakini kocha Robertinho ameendelea kumtumia na kumjengea hali ya kujiamini kwa kufanya naye kikao mara kadhaa.
“Sasa hivi anathibitisha ubora wake katika michuano ya kimataifa kutokana na kiwango kizuri ambacho anaendelea kukionyesha kimataifa.
“Katika michezo miwili Kocha Robertinho alimuanzisha tulipocheza nyumbani na ugenini na kuonyesha kiwango kizuri huku akiisaidia timu kupata matokeo mazuri,” alisema mtoa taarifa huyo.