Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kamati ya Sheria TFF ndio iliyokoroga sakata la Kagoma

Kagoma Saaa Kamati ya Sheria TFF ndio iliyokoroga sakata la Kagoma

Mon, 16 Sep 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Uamuzi wa Shirikisho la Kimataifa la Soka (Fifa) kuzuia shughuli za michezo kwenda katika mahakama za kawaida si tu kwamba ulilenga shughhuli za mpira zishughulikiwe na vyombo vya mpira pekee, bali uamuzi uendane na utamaduni na kasi ya mchezo wenyewe.

Katika mahakama za kawaida shauri laweza kuwasilishwa mezani leo, likaamuliwa mwakani kutokana na taratibu za kimahakama, wingi wa mashauri huku wasikilizaji wakiwa wachache, upande mmoja kutoa sababu kwa nyakati tofauti kuomba usikilizaji usogezwe mbele, mapingamizi na sababu nyingine nyingi.

Pia shauri linaweza likaamuliwa kwa kasoro ndogo tu iliyobainika kisheria wakati tatizo la msingi halijashughulikiwa kutafuta suluhisho la kweli. Mfano kesi yaweza kumalizwa kwa sababu kiapo tu kilikosewa.

Kwa hiyo, kwa sababu nilizozitaja hapo juu, kesi ya kupinga uhalali wa mchezaji inaweza isitolewe uamuzi hadi mwakani, huku mlalamikaji akiwa ameomba zuio la mchezaji kucheza hadi kesi ya msingi imalizwe. Kwa mukhtadha kama huo, masuala ya soka yakiwa yanapelekwa katika mahakama za kawaida, ligi inaweza isichezwe kwa maombi kama hayo madogo madogo ndani ya kesi kubwa.

Nashangaa sasa kwamba hata vyombo vilivyoundwa kushika nafasi ya mahakama za kawaida, sasa zimeanza kufanya shughuli zake kwa utamaduni uleule wa mahakama tulizozikimbia.

Ungetegemea kwamba kamati kama ile ya sharia na hadhi za wachezaji ingeona umuhimu wa kukutana mwanzoni mwa msimu ili kushughulikia utata wote uliojitokeza kwenye usajili ili wakati msimu unaanza kusiwe na mashauri mbele yake yanayoweza kuathiri matokeo ya uwanjani, kwa maana ya timu kucheza bila mchezaji iliyemtegemea msimu huo, timu kupokonywa pointi kwa mechi ambazo mchezaji mwenye kasoro amecheza kama kamati inakuwa imara au mambo mengine yoyote yanayoweza kuibuka.

Na ungetegemea kwamba Bodi ya Ligi Kuu imeweka kanuni ya kulazimisha mashauri yote kuhusu uhalali wa wachezaji yawe yamewasilishwa si chini ya siku kumi kabla ya ligi kuanza ili yatolewe uamuzi na kuwezesha msimu kuanza bila ya kelele zinazoondoa ladha ya mpira na kusababisha vyombo vya haki vya TFF kuonekana vina upendeleo au vinafanya makusudi kwa masuala yanayohusu timu fulani.

Wiki hii baada ya mwanasheria wa Yanga kutoka hadharani kuzungumzia suala la kiungo wa zamani wa Singida Fountain Gate, Yusuf Kagoma, mashabiki wamemshangaa na kutaka Shirikisho la Soka (TFF) limchukulie hatua.

Nilidhani kuwa watu wangeshangaa sababu za suala hilo kutotolewa uamuzi hadi Ligi Kuu inaanza, huku mchezaji ambaye shauri lake liko mezani akionekana uwanjani.

Binafsi najua jinsi Mwanasheria wa Yanga alivyojikinga kisheria kukwepa adhabu ya kushughulikiwa na TFF kwa kosa la kuzungumzia shauri ambalo liko mbele ya kamati kwa ajili ya uamuzi kwa kuwa alichofanya ni kuzungumzia masuala ambayo Yanga ilishughulikia katika kesi hiyo na si kuchambua ushahidi uliowasilishwa na pande zote. Kuchambua ushahidi na kutoa msimamo ni kuingilia mahakama na kujaribu kumshawishi hakimu au kamati kuamua kile unachoona kuwa ni sahihi.

Lakini Mwanasheria wa Yanga hakujikita kuzungumzia ushahidi uliowasilishwa na Singida Fountain Gate na kuulinganisha na wa Yanga, bali ule ambao mtu yeyote angeuona katika hati yao ya kuwasilisha shauri hilo. Ni kama kumsomea mtu hati ya malalamiko yaliyowasilishwa na walalamikaji ambao unaweza kuwekwa hadharani au ukaenda pale mahakamani ukaomba faili na kupewa kulisoma.

Lakini hoja yangu ni kasi ndogo ya kamati ya sharia kushuhghulikia suala ambalo ni la haraka. Kama iliweza kushughulikia suala la Lameck Lawi mapema kabla hata hajagusa uwanja, imekuwaje suala la Kagoma lichelewe.

Kulikuwa na haja gani basi ya kukimbia mahakama za kawaida wakati vyombo vyetu vya haki havifanyi kwa kasi na utamaduni wa mpira wa miguu? Shauri la uhalali wa mchezaji si madai ambayo yanaweza kusubiri taratibu nyingine na kwa muda mrefu kwa kuwa haliathiri timu wala mchezaji kwa haraka.

Lakini suala linalohitaji mchezaji kuanza kutumika au kuondolewa utata wa uhalali wake, linahitaji kasi ili fedha zilizotumika kuwekeza kwake zianze kuonekana kwa kadri mwajiri anavyotaka.

Suala hilo pia lina chembechembe za ukiukwaji wa maadili. Umeanza utamaduni wa kitapeli wa viongozi kuchjukua fedha upande mmoja na baadaye kugeukia dau kubwa. Maana yake kunaweza kukawa na shida ya haraka wakati huo, viongozi wakaamua kuchukua fedha iliyo mbele huku wakiweka sharti ambalo wanajua linaweza lisifuatwe, na baadaye wakachukua dau kubwa na kukata zile fedha walizochukua awali wakati huo washamaliza ile shida ya muda mfupi.

Hilo limetokea kwa Lawi na Kagoma na kautamaduni haka kataanza kukolea kama tulivyotahadharisha awali wakati Feisal Salum alipogoma kuchezea Yanga akidai anataka kuvunja mkataba. Utaduni huo ukaikumba Geita Gold na baadaye Azam FC wakati Prince Dube alipoamua kuvunja mkataba hata kabla ya msimu kumalizika.

Nimeona watu wameanza kurudi mahakamani kudai haki zao kwa kile kinachoonekana vyombo vya haki vya TFF haviwajibiki ipasavyo.

Hatutakiwi kulea uzembe ambao unaweza kusababisha watu wakaona ni bora kwenda mahakama za kawaida kuliko kuendelea na vyombo vya haki vya TFF kwa kuwa vinaonekana haviwajibiki ipasavyo kwa kasi na utamaduni wa mpira wa miguu.

Ni muhimu sana wajumbe wa kamati hizo wakapewa elimu ya kutenda haki kwa kufuata utamaduni wa mpira wa miguu badala ya kutegemea uzoefu wao katika kazi zao za uwakili katika mahakama za kawaida.

Chanzo: Mwanaspoti