Baada ya juzi Jumapili kuiongoza Al Hilal kuilazimisha Simba sare ya bao 1-1 kwenye mchezo wa kimataifa wa kirafiki, Kocha Mkuu wa Al Hilal ya Sudan, Florent Ibenge, ameweka wazi kuwa kwa ubora aliouona ndani ya kikosi cha Simba anaamini wana kikosi cha kufanya makubwa katika Ligi ya Mabingwa Afrika.
Al Hilal juzi Jumapili waliilazimisha Simba sare ya bao 1-1 katika mchezo wa kimataifa wa kirafiki uliopigwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam ambapo mchezo huo ulikuwa wa mwisho wa kirafiki kati ya michezo mitatu ambayo Al Hilal walipanga kucheza kujiandaa na mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Mamelodi Sundowns.
Mchezo huo pia ulikuwa wa mwisho kwa Simba kujiandaa na mchezo wa kwanza wa hatua ya makundi Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Horoya AC ya Guinea.
Ibenge alisema: “Ulikuwa mchezo mzuri kwa pande zote mbili, tulitengeneza nafasi nyingi za kufunga lakini hatukuzitumia na Simba walifanikiwa kusawazisha, lakini jambo la muhimu sio matokeo bali tumepata nafasi ya kuangalia ubora na mapungufu yetu na tutayafanyia kazi kabla ya kucheza na Mamelodi.
“Kuhusu Simba nadhani wana kikosi bora sana, kuna wachezaji wengi wamewaongeza ambao ni wazuri, naamini kwa rekodi waliyonayo na ubora huu wa kikosi bila shaka wana nafasi kubwa ya kufanya vizuri.”
Simba katika Ligi ya Mabingwa Afrika imepangwa Kundi C na timu za Horoya, Vipers na Raja Casablanca.