Ilikuwa ni shoo ya kibabe. Shoo iliyoaacha kumbukumbu tamu kwa mashabiki wa Simba ambao waliishuhudia timu hiyo ikiandika rekodi ya kutinga robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa kishindo ikipata ushindi mnono wa mabao 7-0 dhidi ya Horoya AC ya Guinea.
Simba, imetinga hatua hiyo ikiwa ni mara ya tatu katika misimu mitano, lakini hapo nyuma haikuwahi kutinga kwa ushindi mnono kama huo ambao umeingia kwenye historia ya soka la Afrika na kuiacha Horoya wakishindwa kuamini kilichowakuta katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.
Ushindi huo umeifanya Simba kufikisha pointi tisa baada ya mechi tatu za Kundi C ikiwa nyuma ya Raja Casablanca iliyolazimishwa sare ya 1-1 ugenini mbele ya Vipers ya Uganda.
Kuna mengi yalijiri kwenye mechi hii lakini hapa tumekupa uchambuzi wa kina juu ya kile kilichoipa Simba nafasi ya kupata mabao yote haya, huku Clatous Chama akifanya makubwa kuendeleza rekodi zake tamu ndani ya timu hiyo hasa kwenye michuano ya kimataifa.
MTEGO ULIKUWA HAPA Muda mwingi wa mchezo Simba ilikuwa imeiachia Horoya ichezee mpira hususan eneo la kati.
Ile haikuwa bahati mbaya bali ulikuwa ni mtego ambao Horoya waliingia bila kujua.
Ikiwa Horoya isingekuwa inachezea mpira ingekuwa na maana Simba ingepata ugumu sana kwenye kuwafungua.
Kitendo cha kukubali kuchezea mpira na kuwafanya waende mbele sana kilisababisha kuachwa kwa mianya sana na pale Simba ilipokuwa ikiwapokonya mpira lango lao halikuwa na watu waaozidi wanne hadi watano ambao kiuhalisi hawakuwa kwenye umbo sahihi kwani hadi wao walikuwa wakipanda kwa ajili ya kusaidia mashambulizi.
Wakati huu Simba ilikuwa na idadi kubwa ya wachezaji ambao walikuwa wakiingia kwa kasi sana kwenye boksi, hii ikasababisha mabeki wa Horoya wafanye makosa sana nje ya boksi na ndani hali iliyosababisha waadhibiwe kirahisi.
HOROYA ILIJACHANGANYA Wakati mpira unaanza kabla ya kuruhusu bao, hesabu za Horoya ilikuwa ni kupata walau sare, hili lilionekana kutokana na namna walivyokuwa wamekaa zaidi golini kwao.
Ulikuwa ni mpango mzuri na Simba walionekana kupata tabu kwenye kulifikia goli lao. Lakini faulo ambayo waliitengeneza na kuipa Simba bao ndio iliwaingiza kwenye kiama hiki.
Baada ya kuruhusu bao mpango ukawa ni kutoka kwenda mbele kwa sababu hawakuwa na chakupoteza.
Hii ilisababisha waachie sana mianya na kuwapa mawinga na viungo wa Simba nafasi ya kukimbia nyuma ya safu yao ya ulinzi.
Mwisho wakajikuta Simba wanafika kwenye lango lao kila wakati na kutengeneza mashambulizi.
Kosa kubwa lililofanya Horoya wakumbae na dhahma hii ilikuwa ni kujiachia kwao kwenda kutafuta bao.
MIPIRA HAIKUKAA Pale walipokuwa wanatalawa na kushambulia, Horoya walikuwa wakipoteza mipira mingi sana katikati ya kiwanja na kwenye lango la Simba.
Wakati wanapoteza walikuwa wapo kwenye umbo la kushambulia, hivyo kulikuwa na mianya na nafasi kubwa nyuma yao kwa kuwa timu inaposhambulia, wachezaji wengi huwa nje ya nafasi zao hivyo huwa ina nafasi kubwa ya kuruhusu bao.
Nafasi hizo zilitumia vizuri na Simba katika kuhakikisha wanaiadhibu na walifanikiwa.
SAIKOLOJIA Inawezekana isiwe sababu kubwa sana lakini saikolojia ni moja ya jambo kubwa kwenye mpira wa miguu.
Kama ulikuwepo uwanjani mara kadhaa huenda ulishuhudia hata kwenye benchi la ufundi la Horoya hakukuwa na utulivu, kuna nyakati wachezaji walikuwa wakimfokea kocha na wakawa wanafokeana wenyewe kwa wenyewe.
Kitendo hiki huwa hakina afya kwenye mechi kubwa kama ile kwa sababu hakutokuwa na maelekezo kutoka kwa kocha yanayoweza kuingia vyema kwa wachezaji na hata kocha mwenyewe anakosa utulivu wa kuchambua na kudadavua kisha kutoka maelekezo ya haraka kwa sababu akili yake inawaza vitu vingi kwa wakati mmoja.
SHOO YA CHAMA, BALEKE Mbali ya makosa kadhaa ambayo Horoya iliyafanya kwenye mechii, wachezaji wa Simba walikuwa kwenye kilele cha ubora wao, kuanzia kwenye kutengeneza mashambulizi na kumalizika.
Utulivu kwenye eneo la mwisho ulikuwa umekosekana kwenye baadhi ya mechi lakni jana ulikuwa kwa zaidi ya asilimia 70. Chama alifanya kile ambacho hakuwa anakifanya kwenye mechi ya kwanza kule Guinea.
Shomari Kapombe na Mohammed Hussein walikuwa mwiba sana kwenye kuzuia na kushambulia kupitia pembeni, kila mchezaji alikaba pale alipopoteza.
Mshambuliaji Kibu Dennis, nguvu na kasi yake ilisaidia kupunguza idadi ya mabeki kwa washambuliaji wengine kwani Horoya walitumia zaidi ya mtu mmoja ili kumzuia wakati huo Chama na Jean Baleke wakawa wanaingia wakiwa kwenye ulinzi hafifu.
Safu ya ushambuliaji ya Simba ilipiga mashuti tisa langoni kwa Horoya na saba kati ya hayo yakaingia kwenye nyavu na kuzaa mabao huku mawili tu ndio yakishindwa kupenya.
Hiyo inaonyesha utulivu wa hali ya juu uliokuwepo kwenye lao la ushambuliaji.