Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Hali si shwari Msimbazi, Yanga wana jambo lao na Chama

Chama Best Goal Clatous Chama

Sat, 15 Jul 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Hali si shwari baada ya kiungo mshambuliaji wa Simba, Clatous Chama kudaiwa kutaka limalizana na timu hiyo kwa kigezo cha mkataba kumalizika akisema ana ofa sehemu nyingine.

Chama, ambaye ndiye mchezaji aliyehusika na mabao mengi zaidi ya Ligi Kuu Tanzania Bara msimu uliopita, alisaini mkataba wa miaka miwili na nusu, tangu alipokuja Januari, mwaka jana.

Lakini taarifa zinadai kuwa jeuri ya sasa ya Chama inatokana na mabadiliko ya kimkataba yanayodaiwa kufanywa baada ya kumalizika kwa msumu wa 2012/22, ambayo uongozi wa Simba unadaiwa kupunguza mwaka mmoja.

Sababu za kupunguzwa kwa mwaka mmoja ni kuonekana kuwa na majeraha ya mara kwa mara kwa nyota huyo, huku pia suala la kocha Robert Oliviera 'Robertinho' kutokuwa na mpango wa kumtumia zaidi msimu huu.

Suala la mkataba ambalo linadaiwa kumpa nguvu Chama, ni kipengele cha mkataba uliodaiwa kubadilishwa kueleza mwisho wake ni 2023, badala ya Juni 2024, kama ambao ilipelekwa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).

Taarifa zilianza kusambaa kuanzia jana asubuhi, kuwa Chama alikutana na viongozi kuomba maboresho ya mshahara na ana timu zinamhitaji, hivyo kama hatapata nyongeza basi apate nafasi ya kuondoka.

Gazeti hili lilimtafuta Ofisa Mtendaji Mkuu wa Simba, Imani Kajuna, ambaye hakupatikana kuweka wazi suala hilo linalochagizwa mitandaoni hadi sasa, ingawa alinukuliwa na kituo kimoja cha gazeti jana akifafanua kuwepo kwa mkataba na nyota huyo.

"Chama bado ni mchezaji wa Simba hadi 2024, hilo ndilo ambalo nalifahamu kwa sasa, hizi taarifa nyingine sijui zinatokea wapi, wachezaji wa Simba waliobaki watajiunga na timu kesho (leo) nchini Uturuki," alinukuliwa Kajuna akizungumza na kituo hicho cha redio.

Lakini mmoja wa viongozi wa klabu hiyo, ambaye aliomba hifadhi ya jina lake, alisema kuna utaratibu uliopo tangu Chama ametua nchini, ambao ulikuwa kila mwanzo wa msimu anatakiwa kupewa kiasi fulani cha fedha (hakukitaja).

"Chama alisaini mkataba wa miaka miwili na nusu kuichezea Simba, na hili la kumpa fedha lilianza tangu msimu wa kwanza (Januari 2022), lakini hali imekuwa tofauti kwa sasa, anaziona ni fedha ndogo japo kila msimu huwa zinaongezeka," alisema kiongozi huyo.

Lakini kwa upande mwingine, bado kuna taarifa kwamba nyota huyu alipunguziwa muda wa mkataba, kutoka miaka miwili na nusu hadi mmoja na nusu, ambao ulitakiwa kumalizika mwishoni mwa msimu uliomalizika.

Sakata hili linaibuka kutokana na Chama kuendelea kuonekana jijini Dar es Salaam, akidaiwa kugoma kuondoka na wenzake, jambo ambalo linazua taharuki kwa mashabiki wanaohofia kama atajiunga na mahasimu wao, Yanga.

Kujiunga na Yanga kunatajwa sasa kutokana na Ofisa Habari wa Yanga, Ali Kamwe kunukuliwa jana akisema kuwa usajili wa mchezaji atakayevaa jezi namba sita utakuwa ni 'kilio cha soka nchini', japo hakutaja sehemu ambayo anatoka nyota huyo.

Taarifa kutoka ndani ya Yanga ni kwamba Yanga imejiridhisha juu ya mabadiliko hayo ya mkataba na kwamba sasa wanasubiri muafaka tu kati ya Chama na Simba, kisha baada ya hapo wanataka kufanya kitu kitakachoshtua kwa mashabiki na kuwa na furaha, lakini upande wa pili kwa watani wao wakibaki na makasiriko.

"Kila kitu kipo sawa unajua Chama na tajiri ni watu wanaozungumza sana kwa muda mrefu alichomwambia tu simama katika kile tulichokubaliana ukimalizana nao njoo muda wowote klabuni kwetu," alisema bosi huyo wa juu wa Yanga.

Ingawa mabosi wa Yanga wanafanya siri, lakini Mwanaspoti linafahamu tajiri wao ameshampa ofa kubwa Chama ambayo kama dili hilo litatiki basi anaweza kuwa mchezaji aliyevuna fedha za kufuru kupitia usajili kwa hapa nchini.

Chama ni miongoni mwa wachezaji waliofanya vizuri na Simba msimu uliopita na ambao wanatarajiwa kuipa nguvu kwenye Ligi ya Mabingwa msimu huu, hivyo kama ikitokea amekosekana huenda ikawashtua mashabiki ambao waliwahi kumnunia Kocha Robertinho na kumtaka 'yeye ndiye aingie kwenye mfumo wa staa huyo.'

Simba na Yanga zinaendelea na hekaheka za usajili tayari kwa msimu mpya wa Ligi Kuu Bara na michuano ya kimataifa na tayari wameshashusha silaha kadhaa.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live
Related Articles: