Kama ulidhani kuondoka kwa Saido Ntibazonkiza ndani ya Geita Gold itapata tabu ya upigaji wa penalti, basi umekosea, kwani tayari timu hiyo imepata mrithi wa Mrundi huyo na penalti zinafungwa kama kawaida.
Jofrey Manyasi ndiye aliyebeba mikoba ya Saido kwa sasa pale Geita kwani amekuwa ndiye kinara wa kupiga mipira hiyo na yote kutia kambani.
Geita ni kati ya timu zilizopata penalti nyingi msimu huu ikipata sita kama ilivyo kwa Dodoma Jiji, zikiwamo tano za Ligi Kuu na moja ya Kombe la ASFC na imefunga zote Saido alifunga mbili, Manyasi mbili, huku Offen Chikola na Haruna Shamte kila mmoja amefunga moja moja.
Manyasi alifunga penalti kwenye ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya Ruvu Shooting (Ligi Kuu) na 3-1 dhidi ya Green Warriors katika ASFC, mechi zote zikipigwa Uwanja wa Nyankumbu, Geita.
Manyasi ambaye amedumu na timu hiyo kwa misimu minne sasa alisema siyo bahati mbaya yeye kupiga penalti kwani alianza akiwa Boma FC ya Mbeya na baada ya kuondoka Saido, kocha Felix Minziro amekuwa akimuamini na kumpa jukumu hilo.
“Kocha kaniamini na wenzakei wameniamini, ndiyo aliamua kila penalti ikitokea napiga, hivyo naitumia vizuri kwani unajua tena ndio sehemu ya kumuonyesha kocha ile imani aliyonayo kwangu."
Kiungo huyo mwandamizi kikosi aliwapongeza mashabiki wao kwa kuwaunga mkono katika mchezo wao wa Shirikisho dhidi ya Green Warriors na kufanikiwa kutinga robo fainali huku akitamba kuwa timu yoyote watakayopangwa nayo wako tayari kukiwasha.