Kiungo Hassan Dilunga anaamini mitihani ya Mungu ipo kwa ajili ya kutoa funzo na tafsiri sahihi ya maisha ya binadamu kujua kuwa cheo na afya vinaweza vikabadilika muda wowote.
Anasimulia alivyopata majeraha akiwa kwenye mazoezi na timu yake ya zamani, Simba kwenye Uwanja wa Mo Simba Arena uliopo Bunju akisema: “Ilikuwa kama utani kwani wakati wa mazoezi kila mchezaji anakuwa anapambana kwa ajili ya kumshawishi kocha ili ampange kwenye kikosi chake.
“Ni bahati mbaya, Erasto Nyoni alinikanyaga kwenye goti. Sikutegemea kama ningekaa nje mwaka mzima bila kucheza, tena kipindi hicho kiwango changu kilikuwa kikubwa. Lakini nimejifunza kujua Mungu anaweza akabadilisha chochote katika maisha ya mtu iwe cheo, afya - jua kuna muda vinaweza vikatoweka.”
Katika mahojiano yake na Mwanaspoti, gazeti hili limegundua upole kwa sura, ila jamaa anapenda stori, mcheshi, anachuja mambo kujua kipi anaweza akasema na kipi aachane nacho. Kikubwa zaidi anaamini lolote lililomtokea kwenye maisha yake anaamini Mwenyezi Mungu ameona anastahili.
Japo sio mwepesi wa kufunguka sana na kama sio umakini anaweza akakutoa nje ya maswali, ila anapima ni kipi akizungumze na kipi abaki nacho moyoni.
Anafunguka namna alivyopitia changamoto ya kukaa nje bila kazi, wakati mwingine utani wa mashabiki mtaani akiambiwa hana lolote kaachwa na Simba, lakini yote hayo anayachukulia kama funzo la kumjenga.
MAISHA NJE YA SOKA
Akizungumzia maisha nje ya soka, Dilunga naasema: “Neno maisha ni pana ukiwa na nafasi unaweza ukaona kila kitu umekimaliza, ila baada ya kukaa nje muda mrefu nikiuguza majeraha ndipo nimegundua maisha mengine tofauti na kipindi nacheza.
“Unapopata nafasi ya kufanya kazi yoyote ukiwa na afya njema ni vizuri ukaiwaza kesho yako zaidi kuliko leo. Nitafanya hivyo nikirejea uwanjani.”
Japo ilikuwa ngumu kufunguka kiundani zaidi, anasema wakati mwingine alikuwa anashindwa kuzitazama mechi zinazoendelea za Ligi Kuu Bara kwani zilikuwa zinamjia hisia za kuwepo kazini.
“Nilikuwa nawaacha wenzangu wanaangalia TV sebuleni, mimi naingia chumbani, labda likifungwa bao natoka kuangalia limefungwaje. Ujue kuna wakati unajikuta unajawa na mawazo sana, ndio maana niliepuka kila aina ya kunipa maumivu ya moyo,”anasema.
Anazitaja mechi alizokuwa analazimika kuziangalia ni za Simba ikicheza, Yanga, Azam FC na Singida Big Stars
“Natarajia kurudi uwanjani. Kuna mechi ngumu na za ushindani nililazimika kuzitazama na ukiachilia mbali hilo ila nilikuwa natazama pia Ligi ya Mabingwa Afrika,” anasema.
Akiulizwa ukaribu na wachezaji wenzake kipindi yupo nje umekuwaje? Anajibu: “Pata tatizo ujue uhalisia wa watu dhidi yako, wapo wengi waliokuwa wanakuja kunisalimia na wengine nawasiliana nao kwenye simu kila siku, hata wale ambao sikupata bahati ya ukaribu nao siwezi kuwasema vibaya kwa sababu huenda ndio watakaonisaidia kesho yangu.”
Simba ina mashabiki wa kutosha je anaishi nao vipi mtaani? Anaeleza, “wapo ambao wanaweza wakakukejeli, lakini napaswa kuyavumilia yote kwa sababu kilichoniweka nje ni baada ya kuumia goti na kufanyiwa upasuaji.
“Mtaani kila mtu anasema lake, unasikiliza wanachosema unayaacha hapohapo na maisha mengine yanaendelea, ingawa inafunza kwamba ni vizuri kuishi na kila mtu vizuri. Pia imenipa taswira siku nikitundika daluga uhalisia wa mtaani upoje na kipi ambacho napaswa kukifanya.”
BIMA YA AFYA
Dilunga analiomba Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na Bodi ya Ligi Tanzania (TPLB) kusimamia bima za afya kwa wachezaji ili kunusuru maisha yao.
“Nilijifunza kupitia kwa Gerald Mdamu wa Polisi Tanzania alivyopata shida nikagundua bima ni jambo la muhimu na linalotakiwa kupewa nguvu, msisitizo na wasimamizi wa soka.
“Najiuliza mfano mchezaji wa timu ndogo akiumia nje na timu maisha yake yanakuwa na usalama gani?” anahoji.
Anaongeza: “Mimi nina Bima binafsi, ambayo inaweza ikanisaidia kutibiwa kwa urahisi pindi yanaponitokea majanga.”
MAZOEZI SIMBA
Nyota huyo anafanya mazoezi na timu ya Simba chini ya uangalizi wa daktari ili kutafuta ufiti wa misuli.
“Ni wiki mbili tangu nianze kufanya mazoezi na Simba. Mara ya kwanza nilipokutana na Kocha Mkuu Roberto Oliveira ‘Robertinho’ anasema ana taarifa zangu hivyo napaswa kupambana zaidi kuonyesha uwezo wangu.
“Kuhusu msaidizi wake, Juma Mgunda nafahamiana naye, nimekutana naye kwenye majukumu ya Stars mara nyingi na hata wakati akiitumikia Coastal Union hivyo ni mtu ambaye niko karibu naye,” anasema Dilunga.
Anaongeza kuwa wachezaji wenzake walifurahi kumuona na kumpa moyo wakiamini atarejea tena kwenye kiwango chake.
“Simba ikisafiri kwenye majukumu ya CAF ama wakicheza mkoani nafanya mazoezi na JKT Tanzania. Ndio maana mmenikuta hapa mazoezini leo, yote hayo nasaka utimamu wa mwili ili kuifanya misuli ikunjuke,” anasema mchezaji huyo.
Kabla ya kuonekana Simba na JKT ambako anafanya mazoezi, lakini Dilunga awali alionekana akiwa na kikosi cha Azam huku
akieleza: “Kule nilikwenda kwa huduma ya gym kwa sababu nahitaji mazoezi zaidi ya aina hiyo na sio jambo lingine.”
MAUMIVU MAKALI
Ni miezi miwili imepita tangu afiwe na mtoto wake wa kiume mwenye umri wa miaka minane na alipoulizwa na Mwanaspoti tukio gani limewahi kumuumiza na hatakaa alisahau, uso wake wa furaha ghafla ukabadilika na akatawaliwa na ukimya kama sekunde tatu hivi.
“Yapo mengi yamepita maishani mwangu ila hili la kufiwa na mwanangu nakumbuka kila dakika. Naumia sana kwani moyo wangu unavuja damu, kuna wakati nahisi naota ila ni ukweli. Nilizowea kwenda naye uwanjani, ila napaswa kushukuru kwa kila jambo,” anasema.
Baada ya kuona hisia za huzuni zimezidi kwenye macho yake na mdomo kusitasita kuzungumza maneno mengi juu ya kifo cha mwanaye, waandishi wa makala haya ilibidi wabadilishe stori kumrejesha kwenye mudi nzuri ya mazungumzo.
Na alipoulizwa kwa nini anaonekana hapendi kupokea simu, akainua macho juu kisha akatabasamu na kusema hilo limeingiaje kwenye mazungumzo. Utani wa hapa na pale ukaendelea kisha akakaa sawa na mahojiano yakaendelea.
JESHI NA MPIRA
Usajili wa kujiunga na Yanga msimu wa 2013-2015 ndio ulimfanya avue gwanda, ila alikuwa na sababu iliyomfanya afanye maamuzi hayo kama anavyoeleza “Nilikuwa bado sijaajiriwa, lengo ilikuwa ni kutengeneza maisha yangu, baada ya kupata fursa hiyo sikuona sababu ya kuiacha.”
Alipata bahati ya kusoma kozi hiyo baada ya kuichezea Ruvu Shooting aliyokuwa amejiunga nayo msimu wa 2011-2013.
Timu nyingine alizozitumikia ni Stand United (2015/16), JKT Ruvu Stars (2016/17), Mtibwa Sugar (2017/18) kisha Simba 2018 hadi alipoumia 2021.
Anasema endapo ikipatikana bahati ya kurejea jeshini anatamani kulitumikia taifa kwa njia hiyo.
Nje na hilo anawataja Abdu Suleiman ‘Sopu’ na Kipre Junior wa Azam FC kwamba wanakuja kwa kasi na wanaweza wakafanya makubwa endapo wakikaza buti kwenye majukumu yao.