Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Chama ashtua... Wadau wafunguka

Chama Kiwango Chama ashtua... Wadau wafunguka

Mon, 26 Aug 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Mashabiki wa Simba wamepata mshtuko. Hii ni baada ya mpira mkubwa alioupiga Clatous Chama katika mechi mbili za raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika akiwa na kikosi cha Yanga.

Awali mashabiki hao na baadhi wa klabu ya Yanga walikuwa wakiuponda usajili ya kiungo mshambuliaji huyo kutua Jangwani. Walikuwa wakidai ni mzee na aliyepitwa na wakati, lakini kwa sasa hata vijiweni na kwenye mitandao, upepo umebadilika. Zile kejeli za mashabiki wa Simba na hata wale wa Yanga hazipo tena mtandaoni. Chama anaimbwa tofauti kutokana na kuwashtua waliokebehi.

"Chama amezeeka, hawezi tena kufanya maajabu kama ilivyokuwa misimu iliyopita..." Hayo ni kati ya maneno yaliyosemwa na mashabiki wa soka nchini kabla ya msimu kuanza kumhusu Mzambia huyo.

Kejeli na utani huo ulikuwa katika muktadha tofauti, kwani wapo waliosema hivyo wakiamini Chama mwenye umri wa miaka 33 amezeeka na asingefurukuta tena, lakini wengine walisema hivyo ikiwa ni kama 'maneno ya mkosaji' baada ya kiungo huyo aliyekuwa staa Simba kuwaponyoka kizembe kwenda Yanga.

Maneno hayo ya kejeli na utani yalisemwa na wadau tofauti wa soka lakini wengi walikuwa ni mashabiki wa Simba, baada ya Chama kuikacha klabu hiyo na kusaini mkataba wa mwaka mmoja Yanga.

Wale wa Simba wakimponda na kuona ni bora ametemwa na kwamba Yanga ilikuwa imechukua makapi baada ya Msimbazi kumtumia vya kutosha na kupata mafanikio ikiwa naye. Huku baadhi ya mashabiki wa Yanga, nao waliunga mkono kejeli hizo kwa kuona kama mabosi wa klabu hiyo wamezingua kwa kumsajili kipindi hiki akiwa ameshachoka. Kumbe jamaa alikuwa anawasoma tu na sasa ameacha miguu yake ifanye kazi.

Mzambia huyo kama ilivyokuwa kwa Simba, ndivyo imekuwa kwa Yanga. Mara zote amekuwa akianza msimu kwa gia ndogo, yaani hawashi moto kisawasawa lakini kadri siku zinavyoenda ndivyo balaa lake linazidi kuonekana.

Na kwa sasa ameanza kuonyesha rangi zake halisi akiwa Yanga kupitia mechi hizo mbili za CAF ambazo aliisaidia timu hiyo kupata ushindi wa mabao 10-0 na kuwa klabu ya pili kwa mechi za raundi ya awali kufunga mabao mengi nyuma ya Black Bulls ya Msumbiji iliyopo Kombe la Shirikisho iliyoshinda 11-0.

Chama tayari amethibitisha hilo Yanga baada ya kuanza msimu kwa kupooza na kukaa benchi hadi kufikia baadhi ya watu kuzusha habari kuwa Chama hana furaha katika klabu hiyo, kiungo huyo ameanza kuukumbusha umma bado yupo na moto wake ni ule ule.

Juzi Jumamosi amerejea kwenye ubora wake wakati Yanga ikicheza mechi ya marudiano Ligi ya Mabingwa hatua ya awali dhidi ya Vital'O kutoka Burundi na kushinda kwa mabao 6-0.

Chama aliamka. Katika mabao hayo sita yaliyofungwa na Yanga, Mwamba la LUsaka alihusika na mabao matano akifunga moja na kuastisti mara nne katika mchezo huo.

Baada ya mchezo kumalizika, kiungo mwenzake wa Yanga, Mudathir Yahya alipoulizwa kuhusu ubora wa Chama alijibu maneno mawili tu "We hauogopi?"

Jibu hilo ni ishara tosha ya Chama kuwa kwenye ubora wake. Huenda huko mazoezini anaonyesha ubora mkubwa hali ya kuwafanya kina Mudathir na viongo wengine wa timu hiyo 'kuogopa.'

Kitendo cha Chama kuhusika kwenye mabao matano kati ya sita ya Yanga ni muendelezo tu, kwani katika mechi ya awali dhidi ya Vital'O, alihusika katika mabao mawili akifunga moja katika ushindi wa 4-0.

Kwa sasa ni kwamba Chama amehusika na mabao sita kiati ya 10 katika mechi mbili tu, kwa nini Mudathir asihoji; 'We hauogopi?'

Mabao mawili aliyoyafunga katika mechi hizo mbili dhidi ya Vital'O yamempaisha Chama zaidi na kuendeleza rekodi zake katika Ligi ya Mabingwa Afrika.

Amemeendelea kuwa kwenye orodha ya wafungaji bora 10 wa muda wote wa mashindano hayo akifikisha jumla ya mabao 23 na kukaa nafasi ya saba. Anayeongoza hapa ni staa wa zamani wa TP Mazembe ya DR Congo Tresor Mputu aliyefunga mabao 39.

Aidha Chama anakuwa mchezaji aliyewahi anayecheza Ligi Kuu anayeongoza kwa mabao katika Ligi ya Mabingwa Afrika.

Mabao hayo mawili yamemfanya kumpiku nahodha wa timu ya taifa, Taifa Stars, Mbwana Samatta aliyefunga mabao 21 kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika.

Pia Chama ndiye mchezaji Mzambia mwenye mabao mengi zaidi katika Ligi ya Mabingwa Afrika. Mabao 23 yanamfanya kushikilia rekodi hiyo akiweka gepu la mabao 10 na anayemfuata ambaye ni Reinford Kalaba aliyefunga mabao 13 kwenye michuano hiyo mikubwa Afrika kwa ngazi ya klabu.

WASIKIE WADAU

Kocha wa zamani wa Yanga na mchambuzi wa soka, Kennedy Mwaisabula 'Mzazi' alisema Chama ni mchezaji wa daraja la juu katika Ligi ya Tanzania na anapaswa kupewa heshima kubwa.

"Chama ni mchezaji mkubwa na anstahili heshima. Ni mchezaji anayefanya mambo makubwa, yasiyowezekana kwake yanawezekana. Muda ambao hautarajii afanye jambo flani yeye analifanya kwa ufasaha hiyo ndio sifa yake kuu," alisema Mwaisabula.

Kiungo mshambuliaji wa zamani wa Yanga na Simba, Mrisho Ngassa alisema Chama kujiunga na Yanga ni ushindi tosha kwa klabu hiyo.

"Sasa yupo Yanga na amekuta timu ina viungo wengine bora, hivyo lazima ushinda uwepo lakini pia ni faida kwa benchi la ufundi kwani watakuwa na machaguo mengi. Naamini huo ni mwanzo tu, Chama atafanya makubwa zaidi ndani ya Yanga," alisema Ngassa.

Huyo ndiye Chama aliyetua nchini kwa mara ya kwanza Julai 2018 akijiunga na Simba kutokea Lusaka Dynamos ya kwao Zambia na kudumu hapo hadi mwaka 2021 alivyojiunga na RS Berkane ya Morocco ambako pia hakudumu kwani baada ya miezi sita tu alirejea Simba na kukaa kwa kikosini hapo hadi msimu huu alipojiunga na Yanga.

Chanzo: Mwanaspoti
Related Articles: