Shirikisho la Soka Afrika (CAF), limetangaza zawadi kwa bingwa wa Ligi ya Mabingwa Afrika kuwa ni Dola 2.5Mil (sawa na Sh 5,830,125,000,000 za Kitanzania). Michuano hiyo inashiriki Simba ikiwa Kundi C.
Wakati Simba ikiwekewa kushindania kitita hicho, kwa upande wa Kombe la Shirikisho Afrika ambapo Yanga ipo Kundi D, bingwa atachukua Dola 1.25Mil (sawa na Sh 2,915,062,500,000 za Kitanzania).
Simba wenye pointi katika Kundi C Ligi ya Mabingwa Afrika wakiwa nafasi ya tatu na pointi tatu, leo Jumanne wanatarajiwa kujitupa Uwanja wa Mkapa, Dar, kuvaana na Vipers.
Kesho Jumatano, Yanga walio nafasi ya pili Kundi D Kombe la Shirikisho Afrika, wakikusanya pointi nne, watakuwa wakikabiliana na Real Bamako kwenye Uwanja wa Mkapa.
Wakati huohuo, CAF imesema mshindi wa pili wa Ligi ya Mabingwa Afrika, atapata Dola 1.25Mil (sawa na Sh 2,915,062,500,000 za Kitanzania), atakayeishia Nusu Fainali, atapata Dola 800,000 (sawa na Sh 1,865,640,000 za Kitanzania).
Robo Fainali ni Dola 650,000 (sawa na Sh 1,515,832,500 za Kitanzania), huku nafasi ya tatu na nne katika hatua ya makundi, ataondoka na Dola 550,000 (sawa na Sh 1,282,627,500 za Kitanzania).
Kombe la Shirikisho Afrika mshindi wa pili atachukua Dola 625,000 (sawa na Sh 1,457,531,250 za Kitanzania) na nusu fainali Dola 450,000 (sawa na Sh 1,049,422,500 za Kitanzania).
Robo fainali Dola 350,000 (sawa na Sh 816,217,500 za Kitanzania), nafasi ya tatu na nne hatua ya makundi Dola 275,000 (sawa na Sh 641,313,750 za Kitanzania).