Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Bruno Gomez mambo magumu Simba SC

Image 551 1140x640.png Bruno Gomez mambo magumu Simba SC

Fri, 16 Jun 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Wakati Simba SC ikitajwa kumalizana na Kiungo Mshambuliaji kutoka nchini Cameroon Leandre Willy Onana Essomba akitokea Rayon Sports ya Rwanda, mambo ni magumu kwa Wanamsimbazi hao kwa kufanikisha Dili la Kiungo kutoka nchini Brazil na Singida Fountain Gate FC, Bruno Gomes.

Kiungo huyo aliyekiwasha kisawa sawa msimu wa 2022/23, kwa sasa yuko kwao kwa ajili ya mapumziko, amewekewa ngumu kujiunga na Simba SC baada ya kigogo mmoja kuzuia usajili wake kwa Wekundu wa Msimbazi ambao wamepania kurejesha heshima.

Bruno ambaye amefunga mabao 10 msimu ulioisha, aliombwa na viongozi wa Simba SC lakini bado kumekuwa na ugumu kuweza kuitumikia timu hiyo kutokana na kigogo huyo kuzuia usajili wake.

Mbarazili huyo pia ni pendekezo la Robertinho ambaye aliwaambia vigogo wa Simba SC anamtaka ili akasaidiane na Clatous Chama, Saidi Ntibazonkiza na Mzamiru Yassin katika eneo la kiungo.

Mmoja kati ya vigogo wa Simba SC ambaye hakutaka jina lake kuanikwa hadharani amethibitisha Onana na Gomes wamezungumza nao ili kuwasajili na huenda wakatambulishwa mmoja baada ya mwingine.

“Onana na Gomes ni shabaha yetu lakini kuna ugumu kidogo kwa Gomes kutokana na kipingamizi tulichowekewa,” amesema kigogo huyo na kufafanua; “Tayari winga (Onana) tumemalizana naye ikiwa ni mwanzo wa pazia la usajili kwa kikosi kijacho.”

Aidha imefahamika kuwa Simba SC ipo kwenye hatua za mwisho kumrudisha beki wake wa zamani, David Kameta ‘Duchu’ aliyekuwa anaitumikia Mtibwa Sugar.

Simba SC inaamini miaka miwili ambayo Duchu alipelekwa kwa Mkopo Geita Gold na Mtibwa imetosha kumfanya aimarike zaidi sasa atarejea ili kushindania namba na Shomari Kapombe aliyecheza beki wa kulia kwa muda mrefu.

Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally alithibtisha timu yao msimu huu itachukua mchezaji inayemtaka kwenye timu yoyote.

“Siwezi kuweka wazi tumemsajili nani na nani lakini unachotakiwa kujua ni kwamba kila mchezaji tunayemtaka tutampata bila shida yeyote. Simba SC ni timu kubwa,” amesema Ahmed.

Kwa sasa Simba SC imevunja kambi yake na baadhi ya wachezaji wake wapo timu za taifa huku Kocha Robertinho akiwa tayari kwao Brazil, lakini jana Alhamis (Juni 15) klabu hiyo ilitoa taarifa ya kuachana na baadhi ya watu wa benchi la ufundi na kuwatangazwa wapya walioingia kwa kazi za msimu ujao.

Mabosi hao pia wamepitisha panga kikosini na hadi sasa Augustine Okrah ametangazwa rasmi, huku Ismael Sawadogo, Gadiel Michael, Habib Kyombo, Mohamed Mussa, Beno Kakolanya na Mohamed Ouattara wakisubiriwa nao kutangazwa baada ya kumalizika kwa taratibu za kuagana nao pamoja na baadhi ya watu wa benchi la ufundi.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live
Related Articles: