Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Bosi La Liga aichongea Man City

Javier Tebas Medrano Rais wa Bodi ya Ligi Kuu Hispania ‘La Liga’, Javier Tebas

Mon, 16 Sep 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Rais wa Bodi ya Ligi Kuu Hispania ‘La Liga’, Javier Tebas amefichua kuwa idadi kubwa ya timu zinazoshiriki Ligi Kuu ya England (EPL), zimetoa maoni kuwa Manchester City ipewe adhabu kutokana na makosa 115 yanayoikabili.

Usikilizwaji wa mashtaka hayo 115 yanayoihusu Manchester City utaanza kesho Jumatatu huko England baada ya kusubiriwa kwa muda mrefu.

Manchester City inatuhumiwa na makosa ya ukiukaji kanuni za matumizi ya fedha katika kipindi cha miaka tisa kuanzia 2009 ambayo ikibainika kuhusika nayo inaweza kupewa adhabu ya kushushwa daraja, kupokonywa point na faini za fedha.

Bodi ya Ligi Kuu England iliishtaki Manchester City kwa kushindwa kutoa taarifa sahihi za fedha na pia kutotoa taarifa za malipo ya wachezaji na kocha.

Uchunguzi huo ulichochewa zaidi na chapisho la jarida la Der Spiegel la Ujerumani lililovujisha nyaraka zilizoonyesha utakatishaji wa fedha uliofanywa na wamiliki wa klabu hiyo kupitia udhamini huko Falme za Kiarabu.

Hata hivyo, Man City imekuwa ikijitetea mara kwa mara kuwa haijahusika na makosa hayo na kwa sasa inasubiria kupanda kizimbani kujibu tuhuma zinazoikabili.

Lakini wakati ikijipanga kujitetea kesho, Rais wa La Liga, Tebas ambaye amekuwa mkosoaji mkubwa wa mfumo wa uendeshaji na matumizi ya fedha wa Manchester City, amedai kuwa klabu nyingi za EPL zimeichongea timu hiyo inayonolewa na Pep Guardiola.

“Nimezungumza na klabu nyingi za EPL na karibia zote zinafahamu kwamba City (Manchester) inatakiwa kuadhibiwa.

“Wakati fulani waliachiwa na mahakama ya usuluhishi wa michezo (Cas) kwa suala kesi rasmi. Hata kubatilishwa kwa kifungo walichopewa na Uefa kulitokana na sababu za kiufundi tu,” alisema Tebas.

Tebas amesema amefurahishwa sana kuona klabu za Ligi Kuu England zikiungana kukomesha matumizi ya fedha yasiyozingatia kanuni na miongozo ya soka.

“Walikuwa na umwagaji wa fedha ambao ulikuwa unaharibu soka la Hispania. Hatukuweza kufanya kama wao kwa kuwa tungerudi 2010 ambapo klabu zilipotea kisa madeni,” alisema Tebas.

Usikilizwaji wa mashtaka hayo ya Man City unatarajiwa kufanyika kwa miezi miwili ingawa uamuzi wake hautarajiwi kutolewa hadharani hadi 2025.

Katika kipindi ambacho Man City inatuhumiwa kufanya makosa hayo, ilitwaa ubingwa wa EPL mara tatu ambazo ni 2012, 2014 na 2018.

Chanzo: Mwanaspoti