Bodi ya Wakurugenzi ya Klabu ya Simba, imepanga kukutana kwa ajili ya kulifanyia tathimini Benchi la ufundi la timu hiyo, linaloongozwa na Kocha Mkuu, Mbrazili, Roberto Oliveira ‘Robertinho’.
Hiyo ni baada ya Simba kutoka kufungwa mabao 2-1 dhidi ya Azam katika mchezo wa Nusu Fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam Sports uliopigwa Jumapili kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona mkoani Mtwara.
Akizungumza na Spoti Xtra, Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, alisema mara baada ya mchezo dhidi ya Azam FC, haraka uongozi utakutana kufanya tathimini ya kila kiongozi wa Benchi la Ufundi.
Ally alisema upo uwezekano mkubwa wa kuingiza maingizo mapya ya viongozi wa benchi la ufundi katika msimu ujao wenye maono na kuifikisha pazuri katika michuano ya kimataifa.