Wakati Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally akiibuka na kutamka kuwa matumaini ya wao kuwapoka ubingwa wa Ligi Kuu Bara Watani wao wa Jadi, Yanga yamezidi kufifia mara baada ya matokeo waliyoyapata dhidi ya Namungo FC, straika wa timu hiyo, Jean Baleke amesema ni mapema kutupa taulo.
Simba juzi Jumatano walikuwa wageni wa Namungo kwenye mchezo wa Ligi Kuu Bara uliopigwa mkoani Lindi kwenye Uwanja wa Majaliwa na kushuhudia mchezo ukiisha kwa sare ya bao 1-1, matokeo ambayo yameifanya Simba kufikisha pointi 64, pointi nne nyuma ya vinara Yanga kabla ya mchezo wao wa jana Alhamisi dhidi ya Singida Big Stars.
Katika mchezo wa juzi Jumatano, Baleke aliifungia Simba bao pekee ambalo limemfanya kufikisha mabao nane katika mashindano ya Ligi Kuu Bara tangu asajiliwe kwenye dirisha dogo la usajili.
Mara baada ya mchezo huo, Ally alisema kuwa sare hiyo waliyoipata imewaongezea gepu dhidi ya Yanga waliokuwa katika mbio sawa za kugombea ubingwa wa ligi, hivyo ugumu umeongezeka kwao kupambania taji hilo katika msimu huu.
“Matumaini ya sisi kubeba ubingwa msimu huu yamezidi kufifia. Na tumejitakia wenyewe, kwani tumeshaanza kupunguza gepu kwa mpinzani lakini mpinzani ameongeza gape, hivyo sidhani kama ubingwa utakuwa wetu msimu huu.
“Mwenye kukata tamaa, akate tamaa na mwenye matumaini kwamba bado tunanafasi ya kubeba taji la ligi aendelee kuwa na imani yake,” alisema Ally.
Kwa upande wake Baleke alisema: “Kama timu tunaendelea kupambana tukiamini kila kitu kinawezekana kwa michezo iliyosalia, wajibu wetu ni kushinda mechi zetu na hauwezi kututoa kwenye mbio za ubingwa kwa sasa.
“Tuna michezo mitatu, tutapambana kushinda ili kuwa kwenye nafasi nzuri zaidi kwenye msimamo baada ya ligi kumalizika.”