Kichwa kinamuuma Kocha Mkuu wa Simba, Roberto Oliveira ‘Robertinho’ kutokana na safu yake ya ushambuliaji kusumbuliwa na ubutu wa kutumia nafasi wanazotengeneza.
Katika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu, Simba ikiwa kundi C, imetupia mabao mawili ndani ya dakika 360.
Kwenye mabao hayo, wafungaji ni beki Henock Inonga na kiungo Clatous Chama, wote wakifunga dhidi ya Vipers ugenini na nyumbani.
Ikumbukwe kuwa, washambuliaji wa Simba ni Jean Baleke, Moses Phiri, John Bocco na Habib Kyombo ambao bado hawajafunga.
Ukuta wa Simba umeruhusu mabao manne kwenye mechi nne za michuano hiyo hatua ya makundi, huku ikicheza mechi mbili bila ya kuruhusu bao.
Akizungumza nasi, Robertinho alisema: “Unajua huwezi kupata pointi tatu ikiwa hautafunga, washambuliaji wangu wamekuwa na tatizo hilo la kufunga, lakini tunalifanyia kazi.
“Inabidi ujue kwamba mashindano haya ya CAF ni magumu, nasi tunapambana kufanya vizuri kwa wachezaji wote kufunga. Tunatengeneza nafasi nyingi kwenye kila mchezo, lakini kuzitumia hapo ni tatizo.”