Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Baleke, Boka wakoleza moto Yanga

Bokaaa Baleke, Boka wakoleza moto Yanga

Wed, 28 Aug 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Yanga kesho jioni itakuwa uwanjani kuvaana na Kagera Sugar, huku kocha wa kikosi hicho akichekelea kurejea uwanjani kwa mshambuliaji, Jean Baleke pamoja na beki Chadrack Boka walikosekana katika mechi nne zilizopita zikiwamo mbili za Ngao ya Jamii na za Ligi ya Mabingwa Afrika ikiing'oa Vital'O ya Burundi.

Baleke alikosekana katika mechi nne wakati Boka alikosa michezo ya CAF kutokana na ishu ya usajili, lakini kwa sasa kila kitu kimekaa sawa na kocha Miguel Gamondi amesema kurejea kwa Baleke akishirikiana na kina Prince Dube anaona kabisa mambo yanazidi kuwa matamu Jangwani.

Akizungumza na Mwanaspoti, Gamondi alisema Baleke na Boka ambao hakuwatumia katika mechi mbili zilizopita dhidi ya Vital'O wamerudi na alipanga kuwatumia kesho dhidi ya Kagera, kitu alichoamini kinaongeza mzuka katika mchezo huo wa ugenini kabla ya Ligi haijaenda mapumziko kupisha mechi za timu za taifa.

Gamondi alisema kurejea kwa Baleke ni furaha kwa vile anaamini ushirikiano wake na Prince Dube eneo la mbele utaiongezea Yanga makali.

"Naamini Baleke na Dube kwa timu waliyonayo wanaweza kuwa na wastani mzuri wa kufunga kwa kuwa wanacheza kwa kuzungukwa na viungo bora, safari yetu ya kuanza kutetea ubingwa inaanzia hapo na ili malengo yatimie tunatakiwa kushinda kwa kufunga mabao ya kutosha," alisema Gamondi na kuongeza; "Kurejea kwa Baleke baada ya kukosa mechi zilizopita sasa nitakuwa na washambuliaji wanne Kennedy Musonda, Baleke, Clement Mzize na Dube ambao wote watakuwa na nafasi ya kucheza lakini nataka kuona mabao.

"Nimefurahi sakata la usajili wa Baleke kumalizika, lakini ninachotaka sasa ni mara atakapoanza kucheza mechi za mashindano, apambane na Dube kuongeza idadi ya mabao kwenye safu ya ushambuliaji, kila mmoja anatakiwa kutumia nafasi atakayopata kuipa Yanga mabao ya kutosha," aliongeza Gamondi anaikabili Kagera kwa mara ya pili kwenye Uwanja wa Kaitaba, Bukoba baada ya awali msimu uliopita kutoka suluhu kabla ya kushinda jijini Dar kwa bao 1-0 ziliporudiana.

Chanzo: Mwanaspoti
Related Articles: