Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Azam FC itafute sababu za kuboronga Afrika

Azam Fei Lwanga Blanco 0004 Azam FC itafute sababu za kuboronga Afrika

Mon, 26 Aug 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Wakati mashabiki wa Yanga wakimaliza mapumziko ya mwishoni mwa wiki kwa furaha, wale wa Azam na hasa wadau watakuwa wanakuna kichwa kwa huzuni baada ya timu hiyo, iliyokusanya wachezaji nyota kutoka pembe kadhaa za Afrika na barani Amerika Kusini, kushindwa tena kufurukuta michuano ya Afrika.

Azam, klabu inayomilikiwa na mmoja wa matajiri wakubwa nchini na Afrika, haijakuwa na mwenendo mzuri katika mashindano ya klabu ya Afrika na mafanikio inayoweza kujivunia ni kutwaa Kombe la Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati (Cecafa) mara mbili, yaani 2015 na 2018.

Mafanikio hayo hayaakisi ukubwa wa klabu ya Azam kiuchumi n ahata kimiundombinu, ikiwa klabu pekee yenye uwanja wa kisasa unaokubalika kimataifa na ambao umekuwa kimbilio na klabu nyingi ambazo nchi zao hazina viwanja vinavyofikia viwango vya Shirikisho la Soka la Afrika (CAF) na la Kimataifa (Fifa).

Utajiri wa mmiliki wake unaipa uwezo wa kununua mchezaji yeyote inayomtaka Afrika na hata nje, kununua kocha mwenye ubora unaotakiwa, kuendesha program bora za vijana zinazoweza kuzalisha wachezaji nyota sit u wa timu ya taifa ya Tanzania, bali pia mataifa mengine.

Lakini tangu ianzishwe mwaka 2004, takriban miaka 20 iliyopita, haijawa na mafanikio makubwa katika Ligi ya Mabingwa iliposhiriki 2014 baada ya kutwaa ubingwa wa soka wa Tanzania Bara.

Mwaka huu ilitegemewa ungekuwa wa mafanikio ya angalau kufika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa, nafasi iliyoipata baada ya kushika nafasi ya pili katika Ligi Kuu, lakini hali imekuwa mbaya zaidi baada ya kutolewa raundi ya kwanza ya michuano ya awali kwa kufungwa jumla ya mabao 2-1 na APR ya Rwanda.

Tangu mwaka jana, Azam ilionekana imepania kufuta doa la kufanya vibaya Afrika ilipoanza kukusanya nyota kutoka ndani na nje ya nchi. Mwaka jana ilimsajili Gibril Sillah, mshambuliaji hatari kutoka Gambia ambaye amesaidia kuongeza makali.

Kama haitoshi ikamchukua kiungo mshambuliaji kutoka Yanga, Feisal Salum, maarufu kama Fei Toto, ambaye pia ameifanya safu ya ushambuliaji kuwa moto wa kuotea mbali.

Msimu huu ndio imefanya makubwa zaidi kwa kuimarisha kila eneo. Katika ngome ilimchukua Yoro Mamadou Diaby mwenye miaka 23 raia wa Mali, Frank Tiesse (26), kiungo mshambuliaji kutoka Ivory Coast, Ever Meza (24), kiungo wa kati kutoka Colombia, Jhonier Blanco (24), mshambuliaji kutoka Colombia na Nasor Saadum kutoka Geita Gold ya Tanzania.

Unaweza kusema kikosi kinachokuwa uwanjani hakina tofauti na kile kilichopo benchi la wachezaji wa akiba, ama kwa maneno ya kimpira, ina kikosi kipana.

Hata ikitaka kuweka kambi sehemu yoyote Afrika au barani Ulaya, uwezo wa kiuchumi wa mmiliki utaiwezesha kwenda kokote ambako benchi la ufundi linaona kunafaa

Kwenye benchi inaye Youssouph Dabo, kocha raia wa Senegal ambaye alitokea klabu ya Teungeuth. Bado Dabo anadaiwa mafanikio kwenye timu hiyo yenye makao yake makuu Chamazi, wilayani Temeke. Dabo yuko na Mfaransa Bruno Ferry, kipa wa zamani wa A.S Miquellonnaise ya Ufaransa.

Wawili hao wamekuwa wakitambulishwa kama kocha mkuu kwa nyakati tofauti na kuna wakati Bodi ya Ligi Kuu ilimpa zawadi Bruno ya kocha bora wa mwezi, ingawa sasa Dabo ndiye anatambulishwa kama kocha mkuu, pengine baada ya kumaliza kozi yake ya leseni ya kusimama benchi.

Katika yote hayo unajiuliza “tatizo ni nini?” Ni wachezaji kutokaa pamoja kwa muda mrefu? Makocha kutoweza kutengeneza program ya muda mrefu kutokana na kutojua hadhi yao katika benchi (mara huyu ni kocha mkuu mara yule)? Uongozi kutojua nini kinatakiwa ili timu ifanye vizuri Afrika? Kutokuwa na mfumo mzuri wa uongozi unaojali zaidi uwajibikaji? Kutokuwa na makocha wazuri? Kutoweza kutambua wachezaji wanaoweza kupambana Afrika? Au ndio yale ya kusema “mpira una matokeo matatu; kushinda, kushindwa au sare?” Au kwa lugha rahisi mazoea.

Haya ni baadhi ya maswali ambayo uongozi wa Azam FC unatakiwa kuanza kujiuliza sasa na si zile siasa za kusema “sasa tunageuzia nguvu Ligi Kuu.”

Pengine mmiliki hana mpango wa kuachana na timu, lakini hali hiyo haitakiwi iwafanye viongozi wabweteke kwamba hata ikiboronga vipi, Azam itaendelea kuwepo. Ni lazima matokeo ya uwanjani, na hasa Afrika, yaendane na uwekezaji uliofanywa katika ununuzi wa wachezaji, kuajiri makocha, ujenzi wa miundombinu na ununuzi wa vifaa bora vya kuwawezesha wahusika kufanya kazi yao kwa kiwango cha juu.

Ukiangalia kwa miaka 20 ya uhai wake, muda ambao binadamu anazaliwa na kuanza kujenga mapenzi na kitu au klabu hadi anakuwa haambiwi lolote, Azam haijaweza kutengeneza mashabiki wa kutosha wasioshabikia Simba wala Yanga.

Basi hata wale vijana wenye umri wa kati ya miaka 15 na 20 waliozaliwa Mbagala hadi Chamazi, si wengi wenye mapenzi yasiyotia shaka kwa Azam. Shinikizo la ziada kutoka nje ya uwanja kwenda kwa wachezaji litatoka wapi?

Maana yake muundo wa uongozi haujazingatia ushirikishwaji wa mashabiki, kitu ambacho ni muhimu kwa uhai na uchumi wa klabu yoyote.

Pamoja na Simba na Yanga kuwa na mashabiki wengi kuliko klabu nyingine zote nchini, bado zinaona suala la ushirikishwaji wanachama ni muhimu na juhudi zinaonekana katika idara hiyo, huku Yanga ikiongeza idara hiyo ya ushirikishwaji mashabiki (fans engagement). Hii hatuisikii Azam zaidi ya mikutano ya kawaida na waandishi wa habari.

Hilo ni doa moja ninaloliona katika muundo wa uongozi na uwajibikaji kwa Azam, lakini najua viongozi wakikaa na kujadili kwa kina, na hata kushirikisha wadau, wanaweza kuibuka na program nzuri ya marekebisho na maendeleo ya baadaye barani Afrika.

Kwa kifupi, suluhisho la kuboronga tena kwa Azam, haliwezi kupatikana kwa fikra na Imani, bali uchunguzi wa kina na majadiliano yatakayosaidia kuifanya timu ipate mafanikio yanayolingana na uwekezaji wa wa mmiliki.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live
Related Articles: