Baada ya kuikandamiza Ihefu FC mabao saba ndani ya siku nne, Simba imeendeleza kilio ndani ya timu hiyo ikidaiwa kumalizana na beki wa kushoto wa timu hiyo, Yahya Mbegu.
Simba ilianza kuwapiga Ihefu kwenye mechi ya Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC), mabao 5-0 mchezo uliochezwa Ijumaa na Juzi Jumatatu katika mchezo wa Ligi Kuu Bara imewakanda mabao 2-0.
Mabosi wa Simba ambao walikuwa wanaiwinda saini ya Mbegu ili kuimarisha kikosi chao mapema kwa ajili ya msimu ujao fasta wamemalizana na beki huyo ambaye mkataba wake unamalizika mwishoni mwa msimu.
Mbegu aliyewahi kukipiga Polisi Tanzania tayari amemwaga wino kwa mkataba wa miaka miwili sasa ni rasmi msimu ujao ataanzisha vita ya ushindani wa namba na Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ anayemiliki beki ya kushoto Msimbazi kwa muda mrefu.
Mabosi wa Simba wamemaliza jambo hilo usiku wa kuamkia jana ‘Jumanne’ kabla ya kuanza safari ya kurudi Dar es Salaam tayari kwa ajili ya mchezo wa ligi dhidi ya watani zao Yanga Jumapili.
Chanzo ha kuaminika kutoka ndani ya Simba kimeliambia gazeti hili mambo yamekamilika na uongozi haukutaka kupoteza nauli tena kwa ajili ya kurudi au kumsfirisha mchezaji aweze kusaini mkataba wamemalizana naye.
“Jambo limekamilika mchezaji kamwaga wino wa kuitumikia Simba kwa miaka miwili na ataungana na timu mara tu baada ya msimu kumalizika kwa sababu ajira yake na Ihefu FC inamalizika mwishoni mwa msimu,?? kilisema.
Alipoulizwa na Mwanaspoti juu ya kuwepo kwa dili hilo, Mbegu alikataa na kuweka wazi: “Tunaelekea dirisha kubwa la usajili mambo hayo ni lazima yazungumzwe, mimi bado ni mcheji wa Ihefu FC hadi mwisho wa msimu na mkataba wangu utamalizika.”