Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Watatu wa familia moja wafa wakitoka harusini

RAS Kilimanjaro Na Dereva Wake Wafariki Kwa Ajali.jpeg Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Almachius Mchunguzi.

Wed, 26 Jun 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Wanafamilia watatu waliokuwa wakitoka katika harusi ya kijana wao jijini Dar es Salaam kurejea Rombo, mkoani Kilimanjaro, wamepoteza maisha kwa ajali baada ya gari walilokuwa wanatumia, kuacha njia na kupinduka.

Waliofariki dunia katika ajali hiyo iliyotokea katika eneo la Bwiko, Wilaya ya Korogwe, mkoani Tanga, ni mama wa bwana harusi, dada mkubwa wa familia ya bwana harusi na shangazi yake huku watu wengine wanne wakijeruhiwa.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Almachius Mchunguzi, amethibitisha jana kutokea ajali hiyo na kueleza kwamba wanafamilia hao walikuwa katika gari dogo aina ya Toyota Noah lenye namba za usajili T 979 CZM.

"Ni kweli hao watu walikuwa wakitokea harusini Dar es Salaam kuelekea Wilaya ya Rombo (Kilimanjaro), ambapo walipofika Bwiko, gari lao lililokuwa likiendeshwa na Godfrey Michael (34), ghafla liliacha njia kwenda porini na kupinduka," amesema.

Kamanda Mchunguzi amewataja marehemu hao ni Cecilia Luka, maarufu Kamashu (58), Judith Juma (42), wote wakazi wa Rombo na mwingine alifariki dunia baada ya kufikishwa eneo la mapokezi ya Hospitali ya Rufani ya Mkoa wa Tanga (Bombo).

Kiongozi huyo wa Jeshi la Polisi amesema kuwa majeruhi waliokimbizwa Hospitali ya Bombo kwa ajili ya kupata matibabu walikuwa wanne.

Amewataja majeruhi hao ni Joshua Michael (27), mfanyabiashara, Jackline Masawe (32), Antonio Luka (40) na mwingine aliyetambuliwa kwa jina moja la Carene, wote wakazi wa Rombo.

Amesema majeruhi hao awali walipatiwa matibabu katika Kituo cha Afya Mombo kabla ya kuhamishiwa Bombo kwa matibabu zaidi.

Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufani ya Mkoa wa Tanga (Bombo), Dk. Frank Shega, amesema kuwa Juni 24 mwaka huu, jioni walipokea majeruhi wanne wa ajali hiyo na wakati wakiwa mapokezi mmoja wao aliyekuwa na hali mbaya alifariki dunia kabla ya kufika wodini.

Kwa mujibu wa Dk. Shega, wamewapokea majeruhi ambao ni mtoto mmoja (15) na watu wazima watatu. Amesema kwamba aliyefariki dunia wakati akipokewa mapokezi alikuwa ameumia sehemu ya kichwa na tumboni na alikuwa na mivunjiko mingi.

Dk. Shega, amesema kuwa kutokana na hali zao kuwa mbaya, mmoja ameshapewa rufani kwenda Hospitali ya Rufani ya Kanda ya Kaskazini (KCMC), Moshi.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live