Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Afrika

Nchi

Kijamii

Wanafunzi 10 wanusurika ajali Goba

Wanafunzi 10 Ajali Goba Wanafunzi 10 wanusurika ajali Goba

Wed, 15 May 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Wanafunzi takribani 10 waliokuwa ndani ya basi la shule (school bus) wamenusurika kupata ajali katika eneo la Kulangwa, Goba jijini Dar es Salaam kutokana na ubovu uliokithiri wa barabara katika eneo hilo.

Tukio hilo limetokea asubuhi ya leo, Mei 15, 2024 wakati wanafunzi hao wakichukuliwa majumbani kwao na kupelekwa shule kama ilivyo kawaida, ambapo dereva wa gari lililokuwa limewabeba, alitumia uwezo wa ziada kunusuru gari walilokuwa wamepanda lisipinduke baada ya kukita kwenye shimo kubwa lililopo kwenye barabara hiyo.

"Dereva amejitahidi sana, yaani kama asingetumia uwezo wake pengine tungekuwa tunazungumza mengine sasa hii. Na mimi mwanangu alikuwa ndani ya gari hilo.

"Barabara kwenye mtaa wetu ni mbovu mno kutokana na mvua zilizonyesha, tumeshapiga sana kelele lakini hakuna kinachofanyika," amekaririwa Khalfan Ismail, shuhuda wa tukio hilo.

Kufuatia tukio hilo, dereva kwa kusaidiana na wasamaria wema, walifanikiwa kuwatoa watoto na kuwakalisha pembeni wakati jitihada za kulinasua gari hilo zikiendelea.

Kwa upande wake, dereva wa gari hilo ambaye ameomba hifadhi ya jina lake, amesema ubovu wa barabara hiyo ndiyo chanzo cha tukio hilo na kuziomba mamlaka kuchukua hatua za haraka kabla maafa hayajatokea.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live