Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Simulizi ya mauaji ya mmachinga Dodoma

Mmachingaaaaaaaa Simulizi ya mauaji ya mmachinga Dodoma

Sat, 13 Jul 2024 Chanzo: Mwananchi

Mwenyekiti wa Mtaa wa Muungano kata ya Nkuhungu jijini Dodoma, Nelson Mpolo amesimulia jinsi walivyoukuta mwili wa mfanyabiashara mdogo katika Soko la Sabasaba jijini Dodoma, John Gerald (30) anayedaiwa kuuawa kwa kuchomwa visu na watu wasiojulikana.

Tukio hilo ambalo limethibitishwa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Theopista Mallya, lilitokea usiku wa kuamkia Julai 10 katika Mtaa wa Muungano karibu na klabu ya pombe za kienyeji.

Mpolo aliliambia Mwananchi kuwa alipata taarifa kutoka kwa wananchi kuwa kuna tukio limetendeka mtaani na alipofika alikuta polisi wakiwa wanaendelea na taratibu zao.

“Alikutwa ameshambuliwa na visu zaidi ya kimoja kwenye kifua hicho ndio tunaamini sababu ya kuondoa uhai wake. Shida iliyosababisha mauaji ilianzia klabuni baadhi ya vitu ikiwemo mkanda wa suruali vilikutwa mlangoni,” amesema.

Ameongeza: “Lakini pia purukushani, kwa maana ya mikiki inaonekana ndani klabu hiyo. Wao polisi wanaweza kuunganisha kuwa zile vurugu zilizofanyika ndizo zilizosababisha mtu kupoteza uhai baadaye au ni purukushani za watu wengine wao wanafahamu”

Akimuelezea marehemu Mpolo amesema kabla ya mauti aliishi katika mtaa huo kwa zaidi ya miaka minne, alikuwa mcheshi na mzalendo na alikuwa mshiriki mzuri wa katika shughuli mbalimbali za maendeleo.

Kuhusu tukio hilo, kamanda Mallya amesema Jeradi alikuwa anakunywa pombe za kienyeji na wenzake katika klabu moja ambapo kulitokea ugomvi.

“Kwa maelezo ya awali inasemekana Gerald na wenzake walikuwa wanakunywa pombe za kienyeji kwenye klabu moja kukatokea ugomvi, wakagombana mwenzake akampiga na kitu kizito kichwani. Tunaendelea na uchunguzi kumpata mtu aliyehusika na kumfikisha katika vyombo vinavyohusika”

Amesema matukio mengi ya mauaji na kujeruhi katika Mkoa wa Dodoma yanatokana na ulevi na kwamba matukio mengi wanayoyapokea wakiyafuatilia chanzo ni ulevi.

“Watu wakiacha ama wakipunguza ulevi, tuna uhakika matukio ya mauaji Dodoma kama sio kwisha basi yatapungua kwa kiwango kikubwa,” amesema.

Amesema kwa muda wa wiki mbili matukio matano ya kujeruhi na vifo yaliyosababishwa na vifo yalitokea na chanzo ni ulevi.

Mke aeleza alivyoagana naye

Mke wa marehemu ambaye walioana miezi mitatu iliyopita, Naomi Masima amesema mumewe hakuwa mtu wa ugomvi wala madeni wakati wa uhai wake.

Amesema aliporudi katika shughuli zake za biashara saa 4.00 usiku, hakumkuta mumewe nyumbani hivyo alimpigia simu kumuliza aliko akamweleza yuko nyumbani.

“Mimi sikumweleza kama niko nyumbani, kwa hiyo alivyoniambia yuko nyumbani nikamuuliza nyumba ya wapi? Akanijibu niko nyumbani, nikamwambia niko nyumbani naomba urudi nyumbani. Akaniambia ngoja nitakupigia sasa hivi akakata simu,” anasimulia.

Amesema alivyokata simu, aliendelea kumpigia lakini hakuwa akipokea simu tena wala ujumbe mfupi wa maneno, hakujibu, jambo ambalo lilimfanya kumpigia dada yake.

Naomi amesema hata alipopigiwa na dada yake simu hakuwa akipokea, baada ya jitihada za kumtafuta kushindikana na simu kuishiwa chaji aliiweka tena katika chaji.

“Hadi asubuhi naamka alikuwa hajarejea nikampigia tena simu wifi (dada wa marehemu) kumtaarifu kuwa John hajafika nyumbani. Akaniuliza (wifi) shida ni nini, tuligombana nikamjibu hakuna shida yoyote ile tuliachana kwa amani,” amesema.

Naomi amesema wifi yake akamwambia basi waendelee kumtafuta lakini akiwa anajiandaa kutoka alipata simu ambayo ilimtaka kufika kwa wifi yake.

“Nikachukua pikipiki nikafika kwa wifi akaniambia John (mumewe) amevamiwa na watu, amefariki dunia, nikauliza yuko wapi, nikajibiwa nikaambiwa yuko mochwari,” amesimulia.

Masima amesema maneno anayoyakumbuka wakati wanaagana asubuhi kwenda katika shughuli zao, alimwambia: ”Kazi njema kipenzi na mimi nikamwambia kazi njema na wewe”

Naye Jirani na eneo lililotokea mauaji hayo, Esther Frank amesema aliamka asubuhi kwenda kuchota maji akakuta mtu amelala karibu na mlango wa kuingilia katika nyumba wanaoishi.

“Niliamka asubuhi saa 11 nikienda kuchota maji, nikaona mtu kalala pale chini mimi nikajua labda ni mlevi amelala amepumzika. Lakini baada ya kuchota maji nikaona watu wamekuwa wengi wanaangalia. Kwenda kuangalia kumbe tayari mtu ameshakufa,” amesema.

Chanzo: Mwananchi