Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Shule yatishia usalama wa wanafunzi

Shuleeeeeee Muonekano wa moja ya vyumba vya madarasa Shule ya Msingi Izumbwe

Sat, 13 Jul 2024 Chanzo: Mwananchi

Uongozi wa Shule ya Msingi Izumbwe II Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya, umesema baadhi ya wanafunzi wanasoma katika mazingira magumu kufuatia uchakavu wa miundombinu ya vyumba vya madarasa kuwa na nyufa na mashimo.

Shule hiyo imetajwa kuwa ni miongoni mwa shule kongwe katika Mkoa wa Mbeya ikiwa imejengwa miaka 50 iliyopita huku miundombinu yake ikiwa sio rafiki na kuhatarisha usalama wa wanafunzi na usikivu mzuri kwenye masomo

Akizungumza leo Jumamosi Julai 13 ,2024 Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Ipyana Ndumba amesema shule ina miundombinu chakavu sana iliyosababisha kuta kuwa na nyufa na matundu, hali inayosababisha tatizo la utoro kwa wanafunzi na kutosoma kwa weledi.

"Watoto wanasoma katika mazingira magumu sana miundombinu ni chakavu tunaomba Serikali kuitazama kwa jicho la kipekee ili wanafunzi wasome kwenye mazingira mazuri na kufanya vyema kwenye masomo kwa kuongeza ufaulu,"amesema.

Amesema mbali na uchakavu wa vyumba vya madarasa pia kuna tatizo la huduma hali ambayo inasababisha watoto kutembea umbali mrefu kusaka huduma kutokana na mahitaji muhimu katika huduma za vyoo.

"Tunaishukuru Serikali kwa kuboresha sekta ya elimu kwa kutoa elimu bure kikubwa tunaomba shule za vijijini kukumbukwa kuboreshwa kwani mazingira ya kusomea na kujifunzia ni changamoto."amesema.

Eneo la ndani ya chumba cha darasa ambapo chini ya ubao kukiwa na nyuma.

Akizungumza kwa niaba ya wazazi, Joseph Mwaigaga amesema shule hiyo ni miongoni mwa zilizojengwa kwa nguvu za wananchi kwa lengo la kuwapa maarifa watoto na imezalisha wataalamu wengi ambao wamelitumikia Taifa.

"Ni vyema sasa wadau hata waliosoma katika shule ya Izumbwe kuunga mkono juhudi za Serikali kuchangia ili iweze kufanyiwa ukarabati kwa kutambua ina mchango mkubwa katika maisha yao kwa kuwajengea maarifa"amesema.

Naye Mbunge wa Mbeya vijijini, Oran Njeza amesema atawasilisha changamoto hizo maeneo husika na kuitaka jamii kushirikiana na Serikali kuchangia sekta ya elimu hususan miti kwa ajili ya kuchonga madawati huku yeye akichangia mafuta kwa ajili ya kupasua.

"Nitazungumza na watu wa halmashauri kuona namna bora ya upatikanaji wa rasilimali fedha ili kunusuru madhara kutokea kwa wanafunzi kutokana na changamoto ya miundombinu chakavu "amesema Njeza.

Akitolea ufafanuzi wa changamoto hiyo Kaimu Ofisa elimu msingi, Daniel Mwala amesema tayari Serikali imetenga Sh50 milioni kwa ajili ya ukarabati wa miundombinu chakavu katika shule hiyo ambayo ni miongoni mwa shule kongwe nane ambazo ziko kwenye mpango.

"Hiyo ni miongoni kwa Shule kongwe lakini kuna nyingine ya Irambo iliyojengwa mwaka 1950 sambamba na Igale iliyojengwa mwaka 1930 ambazo zimekarabatiwa kwa gharama ya Sh 90 milioni kwa kila moja, lengo ni kuboresha mazingira wezeshi ya elimu bora kwa watoto "amesema.

Chanzo: Mwananchi