Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Sh4.8 milioni zachangwa matibabu ya mama Sauli, Serikali yajitosa

Dfwadsffeg Sh4.8 milioni zachangwa matibabu ya mama Sauli, Serikali yajitosa

Thu, 8 Aug 2024 Chanzo: Mwananchi

Zaidi ya Sh4.8 milioni zimechangwa papo kwa hapo na waombolezaji, ili kugharamia matibabu ya Hilda Mwasenga ambaye ni mama mzazi wa aliyekuwa mmiliki wa mabasi ya Sauli, Solomon Mwalabila.

Michango hiyo ilifanyika jana jioni Jumatano, Agosti 7, 2024 dakika chache baada ya kumaliza mazishi katika makaburi ya kijijini kwao, Godima wilayani Chunya, Mkoa wa Mbeya.

Mazishi hayo yalihudhuriwa na mamia ya waombolezaji wakiwemo viongozi wa Serikali, kisiasa na wafanyabiashara mbalimbali.

Mwalabila maarufu Sauli, alifikwa na mauti Agosti 4, 2024, Mlandizi, Mkoa wa Pwani kwa ajali ya gari alilokuwa akiendesha mwenyewe kutoka Dar es Salaam kwenda Mbeya kugongwa na lori lililokuwa limebeba mchanga. Ameacha wake watatu na watoto 16.

Kutokana na afya ya mama yake, Mwenyekiti wa Kijiji cha Kibaoni, Joshua Mlambalala kwa niaba ya wafanyabiashara na wachimba madini wilayani humo alifanya changizo ikiwa ni kusaidia matibabu ya mama huyo.

Mlambalala amesema wanafanya hivyo kuunga juhudi za marehemu aliyekuwa anamuuguza mama yake kabla ya kukutwa na umauti.

Amesema Sauli alikuwa mtu mpenda maendeleo na mpenda watu akishiriki shughuli mbalimbali za kijamii na kwamba serikali ya kijiji itaendelea kushirikiana na familia kuhakikisha watoto walioachwa wanakuwa salama.

"Wakati Sauli anakwenda Dar es Salaam alikuwa akimhangaikia mama yake lakini hakuweza kurejea hivyo kwa kutambua mchango wake kwa kile alichofanya kwa jamii tumeona kumchangia mzazi wake matibabu," amesema.

"Hizi pesa ni za wananchi wa Chunya kwa mapenzi yao na tunazikabidhi kwa mtu wa karibu dada yake (Ericka) ambaye atakuwa anapanga matumizi yake na tunaamini itakuwa sehemu salama," amesema Mlambalala.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Chunya, Tamimu Kambona amesema Sauli alikuwa mdau mkubwa wa maendeleo katika kuwekeza katika miradi ya kimkakati hivyo Serikali itahakiksha inakuwa pamoja na familia yake.

"Tumempoteza mtu muhimu sana ambaye alitengeneza ajira kwa vijana na alikuwa mlipa kodi hivyo tunasikitika kumpoteza mwekezaji huyu na tutakuwa karibu na familia," amesema Kambona.

Hata hivyo wakati wa mazishi, mama mzazi wa Sauli, Hilda Mwasenga alishindwa kunyanyuka kuweka shada katika kaburi la mwanaye kutokana na hali yake kiafya.

Akizungumza baada ya mazishi, Mkuu wa Wilaya hiyo, Mbaraka Batenga amesema katika kumuenzi Saulu ni kuendeleza miradi yake aliyokuwa ameanzisha.

"Sauli alifanya uwekezaji akiajiri vijana kupitia mabasi yake na migodi ya dhahabu, hivyo nafsi yangu itafarijika iwapo mali zake zitaendelezwa kwa ajili ya watoto wake," amesema Batenga.

Mkurugenzi wa Udhibiti wa Usafiri wa Barabara kutoka Mamlaka ya Usafiri wa Ardhini (Latra), Johansen Kahatano amesema kifo cha Sauli ni pigo kwa sekta ya usafirishaji na amesisitiza wataendelea kuenzi mema yote aliyoyafanya katika sekta hiyo enzi ya uhai wake.

Amesema katika miaka mitano ya uwekezaji wake katika sekta hiyo, Sauli amekuwa mdau muhimu na ametoa wito kwa wadau wote wa sekta ya usafirishaji kuendelea kuifariji familia yake kwa kuendeleza mema aliyoyafanya ikiwamo ya kutoa ajira kwa vijana.

"Kwa niaba ya Bodi na Wakurugenzi wa Latra, tunatoa pole nyingi kwa familia. Sauli alikuwa mdau mkubwa wa uwekezaji na niombe tuendelee kuenzi yote mema aliyofanya enzi za uhai wake," amesema Kahatano.

Chanzo: Mwananchi