Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Serikali yatoa kauli maandamano Ngorongoro

Ngorongoro 71056561 Serikali yatoa kauli maandamano Ngorongoro

Tue, 20 Aug 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Serikali imetoa ufafanuzi kuhusu madai yaliyotolewa na baadhi ya wananchi wa Ngororo kuwa wanakosa huduma muhimu.

Kaimu Meneja wa Uhusiano kwa Umma wa NCAA, Hamis Dambaya, aliiambia Nipashe jana na kufafanua kuwa, madai ya wananchi hao kwamba hawana huduma nzuri za kijamii si ya kweli kwa kuwa wanapata huduma zote muhimu kama ilivyo kwa Watanzania wengine.

”Huduma zote za msingi wanapata, wanapewa na serikali kama wananchi wengine, kuna shule, vijiji kuna hospitali kila kitu kipo,” alisema Dambaya.

Taarifa aliyotoa kwa umma baadaye ilisema licha ya kuwapo kwa maandamano hayo, shughuli za utalii zinaendelea vizuri na kuwa wanawahakikishia usalama watalii kutoka ndani na nje ya nchi wanaoendela safari zao.

Alisema uwapo wa maandamano hayo unaidhihirishia dunia, jumuiya ya kimataifa, vyombo vya habari na asasi za kimataifa kwamba ndani ya hifadhi hiyo hakuna ukiukwaji wa haki za binadamu na unyanyasaji wa wananchi.

“Mamlaka inawahakikishia watalii wote waliopanga safari za kuja Ngorongoro kuwa serikali itaendelea kusimamia usalama wao wakati wote watakapokuwa ndani ya hifadhi.

“Watalii kutoka ndani na nje ya nchi wameendelea na safari zao za kushuhudia vivutio vya utalii ndani ya hifadhi na serikali inaendelea kuwahakikishia usalama wao,” alisema.

Waandamanaji hao walidai kuwa, wanataka haki ya kurudishwa kwenye orodha ya wapigakura ili washiriki uchaguzi wa serikali za mitaa Novemba, mwaka huu, na Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.

Video mbalimbali zilizorushwa kwenye mitandao ya kijamii zilionesha kundi hilo likiwa limeziba barabara hiyo huku likiimba nyimbo na kulazimisha misafara ya magari yaliyobeba watalii kusimama kwa muda.

Kupitia video hizo, jamii hiyo ilieleza kuwa wamelazimika kufikia uamuzi wa kuandamana kwa amani jana asubuhi kudai serikali iwarejeshee haki zao za msingi ambazo zilizopuuzwa kwa miaka mitatu, kubwa likiwa ni kuondolewa kwenye Daftari la Kudumu la Wapigakura, huku wakiendelea kulipa kodi kama Watanzania wengine.

Mmoja wa wanajamii, Ezekiel Olemangi, alisema wamefuatilia haki yao ya kupiga kura kwenye taasisi husuka ikiwamo Tume Huru ya Uchaguzi (INEC) na Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) bila mafanikio yoyote.

“Lakini hivi karibuni lililoleta shida zaidi ni sisi kuondolewa kwenye orodha ya wapiga kura wa nchi hii, kimsingi tumejaribu kupiga kelele na kufuatilia kwenye taasisi zinazohusika ikiwamo kwenye Tume ya Uchaguzi na TAMISEMI, lakini kila mmoja anarusha mpira kwa mwenzake,” alisema.

Pia, alisema licha ya kuendelea kulipa kodi kama Watanzania wengine kwa miaka mitatu, hadi sasa hakuna mradi wowote wa kuchochea maendeleo umefanyika katika eneo hilo, huku kukiwa na vitisho vingi vyenye kukatisha tamaa ikiwamo askari wa mamlaka hiyo kufanya doria kwenye maboma ya wanakijiji.

Aidha, alisema walifanya juhudi mbalimbali za kuomba kukutana na kuzungumza na mamlaka husika kama vile kuandika barua kwa viongozi wa juu, kuomba kukutana na Rais Samia Suluhu Hassan mara kwa mara bila mafanikio yoyote hivyo wanaona kuwa, njia pekee iliyobaki ni kufanya maandamano ya amani kwa kuwa hawana sehemu yoyote ya kuishi zaidi ya ndani ya eneo hilo.

Awali taarifa inayodaiwa kutolewa na jamii hiyo ilitaja malalamiko yao ni kutoandikishwa kwenye Daftari la Kudumu la Wapigakura hali inayowanyima haki ya kupiga kura na kuwachagua viongozi wanaowataka, kunyimwa umiliki wa ardhi na kulazimishwa kutembea na kadi za kupita katika ardhi yao wenyewe.

“Maandanano hayo ni ishara ya hasira inayoongezeka katika jamii hiyo kutokana na kukosekana kwa maendeleo katika masuala muhimu yanayolenga maisha yao moja kwa moja licha ya kutoa wito kwa serikali mara kwa mara kupatiwa haki hizo,” alisema taarifa hiyo.

Kupitia taarifa hiyo, jamii hiyo ilitoa wito kwa serikali kukaa nao ili kuwasikiliza na kuzishuhulikia kero zao. Vilevile, Watanzania watakuchukulia kwa uzito changamoto wanazopitia na kuunga mkono mapambano yao ya kutafuta haki.

Nipashe ilimtafuta Msemaji wa INEC, ambaye simu yake iliita bila kupokewa wala ujumbe mfupi wa maandishi haukujibiwa.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live