Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Polisi wawaita wananchi kutambua miili ya watu waliouawa Arusha

MAITI YAPOTEA Polisi wawaita wananchi kutambua miili ya watu waliouawa Arusha

Fri, 12 Jul 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha limewataka wananchi wa Arusha kujitokeza katika chumba cha kuhifadhia maiti katika Hospitali ya Rufaa ya Mount Meru kwa ajili ya kutambua miili ya watu waliouawa na wananchi.

Watu hao waliuawa jana Julai 11, 2024 katika matukio mawili tofauti wakiwemo wawili waliokamatwa baada ya kuiba kuku na wengine wawili waliopora simu.

Akizungumza leo Julai 12, 2024, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Justine Masejo amesema vijana hao bado hawajatambuliwa na hivyo amewataka wananchi wa Mkoa wa Arusha kujitokeza kwa ajili ya kutambua miili hiyo.

“Vijana hao wenye umri kati ya miaka 22 hadi 26 wameuawa jana Julai 11, 2024 alfajiri lakini hadi leo hakuna hata mmoja aliyetambuliwa.

“Hivyo, nitumie nafasi hii kuwataka wananchi wa Arusha wajitokeze hapa chumba cha kuhifadhia maiti katika Hospitali ya Rufaa Mount Meru kwa ajili ya kuitambua miili hiyo,” amesema.

Mbali na hilo, amewataka vijana kufuata maadili kwenye jamii na zaidi kutafuta kazi halali za kufanya kuliko kujihusisha na uhalifu hadi kusababisha matukio hayo ya mauaji.

Akizungumzia tukio hilo, Mwenyekiti wa Mtaa wa Muriet, Emmanuel Sanare amesema katika upelelezi wao wamebaini vijana hao siyo wakazi wa mtaa wala jirani na hapo.

“Tumeitana wenyeviti wa kata na viongozi mbalimbali lakini hakuna hata mmoja anayefahamu sura za vijana hao, hii inamaanisha wanatokea mbali,” amesema. Awali ilivyokuwa

Katika tukio la kwanza, watu wawili wameuawa kwa kipigo baada ya kukutwa wakifanya jaribio la kuiba kuku katika Kata ya Muriet.

Mbali na vijana hao, pia watu wengine wawili wameuawa kwa kupigwa na wananchi wenye hasira kali baada ya kukamatwa katika jaribio la kukimbia baada ya kupora simu katika kata ya Kaloleni jijini Arusha.

Mkazi wa Mtaa wa Muriet, Aisha Rashid amesema wananchi wamefikia hatua hiyo kutokana na kikithiri kwa matukio ya wizi na ubakaji, pia, ulawiti mitaani na wakipelekwa polisi, baada ya siku kadhaa wanarudi mtaani na kuendelea na uhalifu.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live