Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ofisa JWTZ ashikiliwa akidaiwa kumvunja mkono mwananchi

Jelaaa Ofisa JWTZ ashikiliwa akidaiwa kumvunja mkono mwananchi

Mon, 16 Sep 2024 Chanzo: Mwananchi

Jeshi la Polisi Mkoa wa Pwani linamshikilia ofisa wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) wa kikosi cha Anga, Luteni Bumija Godwin kwa tuhuma za kumshambulia na kumvunja mkono wa kulia mkazi wa Kijiji cha Msufi wilayani Kibaha, Felisianus Evarist maarufu Msilanga.

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Muhubhwari Msuya amesema Luteni Godwin anatuhumiwa kumvunja mkono wa kulia Msilanga.

“Upelelezi bado kwa kuwa fomu ya PF3 ya Polisi haijajazwa na daktari ametuambia hadi wamalize matibabu yao ya kumfanyia upasuaji ili waijaze na wakimaliza zitapelekwa kwa Ofisi ya Mwanasheria w Mkuu wa Serikali ili watengeneze mashitaka kisha hatua nyingine za kisheria zinafuata,” amesema kamanda huyo.

Akizungumzia suala hilo jana Septemba 16, 2024, Msuya amesema lilitokea Septemba 8, 2024, ambapo Luteni Godwin akiwa na wenzake watatu ambao hawakutajwa majina yao na kati ya hao wawili wakiwa wamevalia sare za jeshi hilo, wanadaiwa walimshambulia Msilanga kwa kumpiga.

Amesema siku hiyo saa 10 jioni, ofisa huyo akiwa na wenzake walifika kwenye shamba lililopo eneo la Msufi Mmoja, ambapo walimkuta mtu mmoja akilima ndipo walimuuliza aliyempa ruhusa, naye akawajibu kwa kuwatajia jina la Obadia.

“Askari hao baada ya kuambiwa hivyo walikwenda hadi nyumbani kwa Obadia na walipofika ukaanza ugomvi mkubwa ndipo wananchi waliamulia ugomvi huo na kisha askari wa JWTZ waliondoka,” amesema kamanda Msuya.

Ameendelea kueleza kuwa, ilipofika usiku askari hao walirudi tena kijiji hapo na walianza kugonga nyumba moja baada ya nyingine kwa wale waliogombana nao jioni ya siku hiyo na kuanza kuwatoa nje huku wakiwapiga ngumi na mteke.

Amesema ilipofika saa 4 usiku askari hao walivunja mlango wa nyumba ya Msilanga wakaingia ndani na kuanza kumshambulia kwa ngumi na mateke jambo ambalo limemsababishia maumivu mwilini.

“Baada ya kufanya tukio hilo, Luteni Godwin alimchukua Msilanga na kumpeleka katika Kituo cha Polisi cha Mlandizi ambapo alipatiwa fomu ya matibabu ya PF3 kisha akampeleka Hospitali ya Mlandizi kwa ajili ya matibabu, wakati huo naye askari huyo alionekana ameumia kwenye kiganja cha mkono wake wa kushoto alitibiwa na kuruhusiwa,” amesema Kamanda Msuya.

Amesema daktari wa hospitali hiyo baada ya kumuona Msilanga ameumia mkono wa kulia alimpa rufaa binafsi ili aende akapige picha ya X- ray na majibu yaliporudi aliandikiwa rufaa ya kwenda katika Taasisi ya Tiba ya Mifupa, Mishipa ya Fahamu na Ubongo Muhimbili (MOI) ambapo alilazwa.

Amesema mgonjwa huyo alilazwa wodi namba tatu na alipofanyiwa uchunguzi na madaktari walibaini mkono wake wa kulia umevunjika, huku ukiwa umevimba ndipo Septemba 12, 2024 aliruhusiwa kwenda nyumbani, lakini akatakiwa kurudi Septemba 17, 2024 kwa ajili ya kufanyiwa upasuaji.

Msilanga aeleza

Akizungumza na Mwananchi akiwa nyumbani kwa ndugu yake Pugu Mnadani Dar es Salaam, Msilanga amedai siku ya Jumapili (Septemba 8) saa 10 jioni alipigiwa simu kuna ugomvi dukani kwa ndugu yake, ndipo alielekea eneo la tukio na alipofika alikuta vurugu kati ya ndugu zake na wanajeshi.

“Niliwasihi wanajeshi waache kufanya vurugu hizo, nikiwaambia hamuwezi mkawanyanyasa raia kama hivi. Basi baada kuamua ule ugomvi uliisha watu tukatawanyika mimi nikarudi nyumbani kwangu.

“Ilipofika saa 5 usiku nikashangaa nagongewa mlango naamriwa nifungue mlango nilivyokataa ulivunjwa,” amedai.

Amedai askari hao walipovunja mlango na kuingia ndani walimtoa na kuanza kumpiga na kumuamrisha waende walikoacha gari lao alipakiwa ndani ya gari hilo akiwa na kijana wake na walipoingia ndani walimkuta shemeji yake naye kakamatwa na walipokuwa njia walilazimishwa kuogelea kwenye bwawa.

“Tulikamatwa mimi, kijana niliyekuwa naishi naye na shemeji yangu kwa pamoja tuliingizwa kwenye bwawa la maji.

“Baada ya hapo kijana wangu walimwachia tukabaki wawili tulipelekwa hadi kituo cha Polisi Mlandizi wakati huo nilikuwa na hali mbaya sana kutokana na kipigo nilichopata,” amedai.

Amedai walipofika kituoni hapo askari Polisi walikataa kumpokea kutokana na hali mbaya aliyokuwa nayo ndipo waliwaamuru askari wa JWTZ wampeleke mgonjwa huyo Hospitali ya Tumbi ambapo alichomwa sindano ya kutuliza maumivu na walifunga mkono wake kwa kutumia maboksi.

Baadaye askari wa JWTZ walimbeba na kumpeleka kituo cha Polisi Mlandizi na walipofika hapo waliwakatalia kumpokea mgonjwa huyo kutokana na hali yake kuwa mbaya na waliamrishwa tena wampeleke hospitali na walimfikisha katika Hospitali ya Mlandizi.

Ameendelea kudai kuwa, alipofika katika hospitali hiyo daktari aliwaeleza askari wa JWTZ kuwa mgonjwa huyo anatakiwa afanyiwe kipimo cha X-ray, ndipo walisema wao hawana hela ndipo wanajeshi walichukua simu yake na kutoa taarifa kwa ndugu zao.

Amedai walipigiwa simu ndugu zake na walipofika hospitalini hapo walimkuta amefungwa pingu kwenye kitanda alichokuwa amelala ndipo walienda katika kituo cha Polisi cha Mlandizi kwa ajili ya kuwachukua askari polisi ili wamfungue pingu hizo.

Kwa upande mwingine mwanakijiji Rashid Ally naye amedai kuwa alivamiwa na wanajeshi hao wakati anatoka kazini, ambapo walimuweka chini ya ulinzi na kuanza kumpiga kwa kutumia rungu huku wakimweleza awaambie alipo bosi wake (hakumtaja).

“Wakati wakinipiga, alikuwepo mjumbe na wanajeshi wanne wakanichukua na kunipeleka kwa Msilanga ambaye shemeji yake nilishuhudia wakimpiga kwa rungu sehemu mbalimbali ya mwili wake kisha tukawekwa chini ya ulinzi pamoja na kijana wake Msilanga.

“Tulichukuliwa na kupelekwa maeneo ya Soga karibu na kituo cha treni ya mwendokasi wakati huo ndugu yangu alikuwa ameumizwa sana wakatuingiza ndani ya bwawa la maji,” amedai.

Kwa upande wake, Bertha Mkomo ambaye ni shemeji yake Msilanga anayeishi Pugu Dar es Salaam, amedai alipopewa taarifa alikwenda kituo cha Polisi Mlandizi akafungua kesi ya shambulio la mwili namba MRZ/RB/2076/2024.

Naye mjumbe wa eneo hilo, Thomas Balisidya amedai siku hiyo saa 4 usiku akiwa amelala ghafla aligongewa mlango na alipotoka nje aliwakuta wanajeshi ambao walimlazimisha waende naye kwenye kazi.

Chanzo: Mwananchi