Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Moto unavyosababisha hasara Tanesco Simanjiro

Umeme Ys (4).jpeg Moto unavyosababisha hasara Tanesco Simanjiro

Mon, 26 Aug 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Shirika la umeme (Tanesco) Wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara, limelaani kitendo cha baadhi ya wakazi wa eneo hilo kuharibu miundombinu kwa kuchoma moto.

Meneja wa Tanesco Wilaya ya Simanjiro, Sixmund Mosha ametoa kauli hiyo leo Jumatatu Agosti 26, 2024 wakati akizungumzia uharibifu uliofanyika kwenye miundombinu yao.

Mosha amesema suala la uchomaji moto limeathiri nguzo za Tanesco zinazozunguka maeneo ya kijiji cha Lorbene Kata ya Naberera, hivyo kusababisha hasara, kwani usambazaji wa nishati hiyo katika vijijini hivyo umetatizwa.

"Siku za hivi karibuni kumezuka mtindo wa uharibifu wa miundombinu inayosababishwa na moto unaowashwa maeneo mbalimbali ya Wilaya ya Simanjiro," amesema.

Mosha ametoa rai kwa viongozi wa Serikali za vijiji, taasisi, misikiti, makanisa na wote watakaofikisha ujumbe wa kuzuia wanajamii wanaowasha moto maeneo ambayo kuna miundombinu ya Tanesco.

"Ikumbukwe miundombinu hii ni ghali na ina changamoto za kuirejesha, tuwajibike sote kutoa elimu na kukemea vitendo hivyo visivyofaa katika jamii," amesema Mosha.

Amesema kila mmoja anapaswa kuwa mlinzi wa mwenzake kwenye jamii na kupiga vita uchomaji moto holela unaosababisha kuunguza miundombinu.

Mkazi wa wilaya hiyo, Emmanuel Mollel amesema baadhi ya watu wanaosafisha mashamba mapya ndiyo wanasababisha hali hiyo kwa kuchoma moto maeneo bila tahadhari.

"Watu hao wanapochoma moto maeneo hayo hushindwa kuzima na kusababisha kuungua kwa mashamba ya majirani na miundombinu hiyo ya Tanesco na kusababisha hasara kubwa," amesema Mollel.

Hata hivyo, ameeleza endapo watu hao wakichukuliwa hatua, ikiwemo kubanwa ili walipe hasara waliyosababisha itawapa funzo na kuchukua tahadhari.

Mkazi mwingine, Elizabeth Lengenyi amesema jamii inapaswa kuwa makini na uchomaji moto holela kwenye mashamba, ili kuepusha kuungua kwa miundombinu hiyo.

Amesema mtu mmoja anaweza kusababisha watu wengi wakapata hasara kutokana na umeme kuzimika na pia Taifa kwa ujumla kwa kununua vifaa vipya vya umeme.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live